Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

JENGEENI UWEZO WATAALAMU WA AFYA KUPUNGUZA VIFO VITOKANAVYO NA UZAZI MKOANI MARA

Posted on: June 24th, 2024



Na WAF – Musoma, Mara


Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred amewataka watoa Huduma na Wataalamu wa Afya wa Mkoa huo kushirikiana kwa ukaribu na Madaktari Bingwa wa Rais Samia kwa kipindi cha siku tano watakazokuwepo Mkoani hapo ili Kuhakikisha wanapewa ujuzi utakao saidia kuboresha kila eneo hususani kupunguza vifo vya Mama na Mtoto, watoto wachanga vitokanavyo na uzazi


Kanali Alfred ametoa agizo hilo Juni 24, 2024 Mkoani Mara wakati wa mapokezi ya Madkatri bingwa wa Rais Samia, ambapo amesisitiza Watoa huduma na Wataalam wa Afya Mkoani hapo kuweka mazingira wezeshi yatakayowawezesha kujengewa uwezo na Madaktari Bingwa wa Rais Samia ili Wananchi wa Mkoa huo na Maeneo ya Jirani kuepuka adha ya kufuata huduma mbali na kuokoa Fedha, Muda na Uhai.


“Takwaimu za Vifo vitokanavyo na uzazi bado haziridhishi, Hivyo niombe sana Watoa huduma na Wataalam wa Afya wa Mkoa wa Mara kushirikiana na timu hii ya Madaktari Bingwa kuhakikisha mnaboresha kila eneo linaloonekana kuchangia uwepo wa vifo kwenye vituo vyenu” amesema Kanali Alfred


Kufuatia takwimu za Vifo vya wamama wajawazito na watoto wachanga katika mkoa huo Kanali Alfred amesema kampeni ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia ndio Mwarobaini wa tatizo hilo na kuagiza wataalam na watoa huduma za afya Mkoani hapo kusimamia vyema utekelezaji wa kampeni hiyo kwa kuhakikisha wanaweka mazingira Rafiki Kunufaika kiujuzi na maarifa na ujio wa kampeni hiyo.


“Wataalamu wetu wa Mkoa wa Mara tumieni vizuri fursa hii kupata ujuzi ili Madaktari Bingwa wa Rais Samia watakapoondoka basi mbakiwe na uwezo wa kutoa huduma za Umahiri hata kama sio kwa kiwango chao lakini muwe mmefikia kwenye kiwango Fulani” amesema Kanali Alfred


Aidha Kanali Alfred ameagiza kuendelea kwa matangazo ya kuwaita Wananchi, wagonjwa na wenye shida mbalimbali zinazohitaji huduma za kibingwa ili waweze kunufaika na uwepo wa kambi hiyo katika wilaya zote za Mkoa wa Mara maana wao ndio walengwa.


“Nitoe wito kwa wananchi wote kutumia nafasi hii kujitokeza kwa wingi, wale wote wenye matatizo mbalimbali ambao walikuwa wanapanga kusafiri kwenda kwenye Mahospitali makubwa ikiwemo Bugando na mahospitali mengine sasa wasiwe na wasiwasi wasogee tu kwenye hospitali zao za Wilaya watapata huduma za kibingwa, Mhe Rais kwa mapenzi makubwa amewasogezea wananchi wote huduma hii muhimu kwelikweli kwa ukaribu zaidi, tutumie vizuri fursa hii nenda hospitali ukakutane na mabingwa utakuhudumia na utasaidika” amesema Kanali Alfred