Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

HUDUMA ZA MATIBABU YA SARATANI KUENDELEA KUBORESHWA NCHINI.

Posted on: October 4th, 2024


Na WAF, DAR ES SALAAM

Ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini Marekani imeendelea kuzaa matunda, kufuatia makubaliano ya kuanzisha kituo cha ubora wa huduma za saratani barani Afrika, kitakachojengwa mjini Dodoma.

Hayo yamejiri kwenye ujio wa Mkurugenzi wa Mass General Brigham Global Advisory Dkt. Smail Ait Ali, kutembelea Taasisi ya Saratani Ocean Road na Hospitali ya Benjamin Mkapa akiongozwa na mwenyeji wake Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, ambapo wamekubaliana kuweka mipango ya kimkakati na uundaji wa ushirikiano wa kimataifa wa huduma za afya katika Mass General Brigham, shirika kubwa la afya lenye makao yake Massachusetts, Marekani.

Dkt. Smail amebainisha kuwa mara baada ya kukamilika kwa jengo maalum la kuhudumia wagonjwa wa saratani itafungwa mashine ya "proton therapy" yenye thamani ya shilingi bilioni 178 ambayo itakuwa msaada mkubwa si tu kwa Watanzania, bali kwa waafrika wengine, kwani itapunguza rufaa za nje ya nchi kwa matibabu ya saratani.

Akifafanua juu ya mradi huo ambao utafungwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema mradi huo ni matokeo ya juhudi za Rais Samia kuvutia uwekezaji wa kimataifa kwenye sekta ya afya, akieleza kuwa lengo ni kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha tiba barani Afrika, kama inavyovutia watalii kwa wanyamapori.

Dkt. Mollel ameeleza kuwa mashine hiyo itasaidia kupunguza rufaa za matibabu nje ya nchi na pia kuongeza mapato ya kigeni kwa kuvutia watu wengi kutoka mataifa mengine ya Afrika.

"Marekani imekubali kujenga kituo hiki cha ubora na kufunga mashine hii ya kisasa ambayo itapatikana Tanzania pekee barani Afrika," amesema Dkt. Mollel, na kuongeza kuwa

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dkt. Julius Mwaiselage, amesisitiza umuhimu wa mradi huo kwa Tanzania, akisema kuwa unaiweka nchi kwenye ramani ya kimataifa katika matibabu ya Saratani.