Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

HUDUMA ZA AFYA YA KINYWA NA MENO ZIMEIMARIKA

Posted on: February 21st, 2024



NA: WAF, Mara

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na *Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan*, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeendelea kuboresha Huduma za Afya ya Kinywa na Meno kwa kusimika viti vya kisasa vya kutoa huduma za kinywa na meno.

Hayo yamesemwa na Dkt. Magembe leo Februari 21, 2024 katika ziara yake akiwa Mkoani Mara alipotembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara (Kumb. Mwl. Julius Kambarage Nyerere) huku akisisitiza umuhimu wa elimu katika kuboresha afya ya kinywa na meno na kuepuka kung'oa meno ya watu pasipo na ulazima.

"Matatizo ya afya ya kinywa na meno yamekuwa yanaongezeka lakini mengi yanaweza kuzuilika endapo wataalamu mtachukua hatua za makusudi kutoa elimu mashuleni, Kliniki ya mama na mtoto na kupitia vyombo vya habari ili kuwafikia watu wengi zaidi na kuhakikisha wanajua jinsi ya kutunza meno yao na afya ya kinywa kwa kwa ujumla”, Amesema Dkt. Magembe

Aidha, amewapongeza wataalamu hao kupunguza idadi ya wananchi wanaong'olewa meno kwa zaidi ya asilimia 80 baada ya kupata viti vya kisasa vya matibabu ya meno.

"Nawapongeza sana, nimeangalia takwimu zenu awali mlikuwa mnang'oa meno takribani asilimia 95 ya wagonjwa wote lakini baada ya kupata mashine za kisasa, sasa hivi wanaong'olewa meno ni asilimia 5 hadi 10, haya ni mapinduzi makubwa. Si sawa kuwafanya watu vibogoyo, wanakosa kujiamini wakati wanaongea au kucheka"

Katika Mkoa wa Mara, Serikali ya awamu ya Sita imenunua viti vya kutolea huduma ya kinywa meno vipatavyo 15 kuanzia vituo vya Afya ndani ya kipindi cha miaka mitatu.