Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

HOSPITALI ZA RUFAA ZOTE NCHINI ZIJENGWE KWA KUFUATA ‘MASTER PLAN’

Posted on: December 30th, 2023

Na. WAF - Arusha

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ameagiza Hospitali zote za Rufaa za Mikoa nchini kujengwa miundombinu yake kwa kufuata ‘master plan’ na kuacha kujenga majengo madogo ya chini kama vibanda ili kupunguza gharama za uendeshaji kwa Serikali na usumbufu kwa wagonjwa.

Waziri Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo leo Disemba 30, 2023 wakati akizungumza na watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha baada ya kufanya ziara katika Hospitali hiyo.

“Nimesikiliza maono yenu na matarajio yenu mnataka kuanzisha maswala ya Kemotherapi, jengo la OPD sasa kabla hamjaendelea nataka mzingatie ‘master plan’ ya mejengo ya Hospitali.” Amesema Waziri Ummy

Amesema, ifike wakati tuachane na mambo ya vibanda vibanda kila sehemu, siku hizi unaweza ukawa na jengo moja tu ambalo huduma zote zinapatikana katika jengo hilo ili kupunguza kharama za umeme, maji pamoja na gharama nyingine za uendeshaji.

Aidha, Waziri Ummy amesisitiza matumizi ya Telemedicine kwa ajili ya kuwajengea uwezo watumishi na kuwajengea uwezo wataalamu wengine katika ngazi ya Wilaya pamoja na vituo vya Afya ili kurahisisha utendaji wao wa kazi.

Pia, Waziri Ummy ameahidi kuwapelekea Kipashajoto cha mtoto (Baby Warmers) 11 katika Hospitali hiyo ya Mount Meru angalau vifike 14 kwa ajili ya kuokoa watoto wachanga wanaopata changamoto za kiafya.

“Mhe. Rais ameshaelekeza anataka huduma bora za Afya zitolewe kwa Watanzani kwa kuwa ameshatoa fedha kwa ajili ya vifaa pamoja na dawa hivyo ni jukumu letu sisi wasimamizi na watendaji kutoa huduma bora za Afya.” Amesema Waziri Ummy.