Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

DKT. MOLLEL - ELEKEZENI FEDHA NYINGI KWENYE SHUGHULI ZA MAPAMBANO DHIDI YA UKIMWI

Posted on: March 15th, 2022



Na WAF - Dar Es Salaam.

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amewataka Wataalam wa Sekta ya Afya pamoja na Wadau wa Maendeleo wanaoshughulikia Masuala ya Ukimwi chini ya Programu ya PEPFAR kuelekeza fedha nyingi zaidi kwenye shughuli za utekelezaji wa afua za mapambano dhidi ya Virusi Vya Ukimwi.

Dkt. Mollel amesema hayo kwenye kikao kazi cha uwasilishaji wa Mpango wa Taifa wa utekelezaji wa shughuli za mapambano dhidi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) kilichowakutanisha kwa pamoja Serikali na Wadau mbalimbali wa masuala ya Ukimwi chini ya programu ya PEPFAR.

"Tunatambua kuwa mnasaidia Serikali katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Ukimwi na mnapata fedha kutoka sehemu mbalimbali ila tunataka fedha hizo mnazopata nyingi mzielekeze kwenye utekelezaji wa shughuli za mapambano na kupunguza yale ambayo siyo ya ulazima" amesema Dkt. Mollel.
Dkt. Mollel amesema kuwa katika kipindi cha miaka 19 ya ushirikiano baina ya Serikali ya Marekani na Tanzania chini ya Programu ya PEPFAR, Tanzania imeweza kupata Fedha za Kimarekani kiasi cha Shilingi Bilioni 5.4 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za mapambano dhidi ya VVU.

"Leo hii tunazo taasisi mbalimbali zisizo za Serikali zinazopata fedha kutoka sehemu tofauti tofauti kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali katika Sekta ya Afya, tunawataka kuona wanavyovifanya kuonekana na mguso katika jamii ya Watanzania" amesema Dkt. Mollel.

Aidha Dkt. Mollel ameishukuru Serikali ya Marekani na Wadau wa Maendeleo kwa kuendelea kufadhili shughuli za mapambano dhidi ya VVU kupitia programu ya PEPFAR na kusema kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano, uratibu na kuongeza rasilimali zaidi katika mapambano dhidi ya VVU.

Kwa upande wake Balozi wa Marekani nchini Tanzania Balozi Donald Wright amesema kuwa Serikali ya Marekani inafurahia ushiriano bora uliopo baina yake na Tanzania na kuhakikisha kuwa wataendela kushirikiana na Tanzania katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Ukimwi.