DKT MBWANJI AIPONGEZA SERIKALI UWEKEZAJI MKUBWA WA WATAALAM AFYA YA MACHO NCHINI
Posted on: August 5th, 2025
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya Dkt. Godlove Mbwanji amesema Wataalam wabobezi wa upasuaji wa mtoto wa jicho nchini wanaoendelea na zoezi la upasuaji wa ugonjwa huo katika kambi ya maalum ya upasuaji wa mtoto wa jicho katika Kituo cha Afya Isimani Mkoani Iringa ni matokeo makubwa ya uwekezaji wa serikali katika utaalamu wa eneo hilo unaopaswa kupongezwa sana.
Akiongea na vyombo vya habari mara baada ya ujumbe wa Shirika la Hellen Keller kuzuru Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa mapema leo Julai 5, 2025 Dkt. Mbwaji amesema kimsingi Shirika hilo linatoa msaada wa kifedha lakini wataalamu wa upasuaji wanatoka katika hospitali za serikali zilizopo Kanda ya Nyanda za juu kusini.
Dkt. Mbwanji ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Iringa kutumia fursa ya uwepo wa madaktari Bingwa wa upasuaji wa mtoto wa jicho kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hiyo ambayo kimsingi imewaondolea changamoto ya kusafiri umbali mrefu na kuepusha gharama kubwa ambayo wangetumia kughalimia matibabu hayo katika hospitali za Rufaa.
Naye Dkt. Greater Mande Afisa Mpango wa Taifa wa Huduma za Macho Wizara ya Afya amesema kuwa kambi hii siyo tu ya kutoa huduma za kitabibu bali pia ni inatoa fursa kwa watoa huduma za Afya walioko katika kambi hiyo kujiendeleza na kupata uzoefu katika hutoaji huduma za upasuaji wa mtoto wa jicho watakapo rejea katika vituo vyao vya kazi.
Aidha Dkt. Greater Monde ameongeza kuwa Shirika la Hellen Keller lina mchango mkubwa katika kutoa vifaa tiba katika vituo vya afya nchini vinavyotoa huduma za afya ya macho ikiwemo Hospital za Almashauri na zile za Rufaa za Mkoa.
Wakati huo Dkt.Stephen Nyamsae ambaye ni Dkt. Bingwa wa Macho aliyeko kambini hapo amesema lengo la kambi hiyo ni kufanya upasuaji kwa wagonjwa takribani 600 hadi 700 kwa siku saba akiongeza kuwa nje ya upasuaji wa mtoto wa jicho pia wanatoa tiba kwa wagonjwa wenye changamoto nyingine ya macho.
Huduma ya upasuaji wa mtoto wa jicho inaendelea kwa siku saba katika kituo cha Afya Isimani Mkoani Iringa na matibabu hayo yalianza tangu Jula 3, 2025 na yatahitimishwa tarehe 9, Julai 2025 kwa wakazi wa Iringa kuendelea kujitokeza kwa wingi kupata huduma hiyo.