Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

DKT. JINGU AGUSWA NA MICHANGO YA WADAU KUHUSU BIMA YA AFYA KWA WOTE

Posted on: October 31st, 2024

Na Waf - Arusha,

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu amesema ameguswa na michango inayotolewa na wadau mbalimbali wa sekta ya Afya kuhusu Bima ya Afya kwa Wote, kutokana na jinsi wanavyojitoa kuchangia kwa kutoa mapendekezo, maoni pamoja na kueleza uzoefu kutoka nchi nyingine ili kuhakikisha kuwa mpango huu unatekelezwa kwa usahihi.

Dkt. Jingu amesema haya Oktoba 31, 2024 katika Kongamano la Bima ya Afya kwa Wote na Jukwaa la Kitaifa la ugharamiaji wa Huduma za Afya linaloendelea katika Ukumbi wa wa Mikutano wa Kimataifa(AICC), jijini Arusha.

Dkt. Jingu amesema ni dhahiri kuwa wote tuko safari moja kwani kazi ya Wizara ya Afya ni kuratibu, hivyo ni jukumu letu sote kuhakikisha kuwa tunafanikiwa kwa pamoja.

"Hatupaswi kuruhusu kushindwa, hivyo kama tulivyoanza pamoja lazima tufanikishe jambo hili kwa pamoja," ameeleza Dkt. Jingu.

Amesema pia kuwa anatambua kuwa wao ni timu ya Bima ya Afya kwa Wote, hivyo katika kila hatua watoe michango yao kwa vitendo ili kufanikisha utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote.

"Jambo hili si la Serikali pekee bali wahusika pia ni wadau wa maendeleo, asasi za kiraia pamoja wadau katika maendeleo ya afya, hivyo kila mwananchi anahusika," amefafanua Dkt. Jingu.

Awali akimkaribisha Katibu Mkuu, ikiwa ni siku ya tatu ya kongamano hili ambalo litahitimisha Novemba1, 2024 Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Tumaini Nagu amemshukuru Katibu Mkuu kwa wazo alilolitoa la kukutana na wadau ili kujadiliana kwa pamoja na kupata maoni ya wadau jinsi ya kutekeleza Bima ya Afya kwa Wote.

Wadau wapatao 300 kutoka ndani na nje ya nchi wameshiriki katika Kongamano hilo la siku nne lililoanza Oktoba 29, 2024.