Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

CHUO CHA AFYA, SAYANSI SHIRIKISHI MOROGORO KUTOA ELIMU YA MASAFA

Posted on: April 30th, 2025

Na WAF, Morogoro

 

Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga kutoka Wizara ya Afya Bw. Saturine Manangwa ameutaka uongozi na Wanafunzi wa chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi, Morogoro kutunza miundombinu na vifaa vilivyotolewa ili kutoa mafunzo ya elimu ya masafa kwa wanafunzi na watumishi wa sekta ya Afya ili kuendelea kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa jamii.

 

Bw. Manangwa ameyasema hayo Aprili 30, 2025 mkoani Morogoro wakati akipokea na kufungua jengo la kituo cha mafunzo ya elimu masafa lililofadhiliwa na Shirika la PATH (Program for Appropriate Technology in Health), akimwakilisha Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe, pamoja na kukabidhi vifaa tiba kwa hospitali tatu (3) ambavyo vitasaidia kuboresha huduma za oksijeni.

 

Amesema uwepo wa kituo hicho kitasaidia wanafunzi na hata watumishi wa afya kupata mafunzo kwa njia ya mtandao wakiwa mbali na kukuza ujuzi na ufanisi wa utoaji wa huduma kwa watumishi hao.

 

“Ninapongeza ubunifu huu ambao umefanywa chuoni hapa, ni dhahiri  umekuja wakati mwafaka, Wizara ya Afya imeufanya mkoa wa Morogoro kuwa sehemu ya kutoa mafunzo ya masafa pia utoaji wa mafunzo kwa watumishi wa sekta ya Afya kwa njia hii kuwa  endelevu kwani  itapunguza gharama na kuleta ufanisi kwa watumishi na wanafunzi pia,” amefafanua Bw. Manangwa.

 

Bw. Manangwa amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau imeweka mikakati ya kuwezesha vyuo vilivyopo Kanda ya Mashariki kuanza kutoa mafunzo ya elimu ya masafa na kuitaka hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro kukifanya chuo hicho kama taasisi iliyo chini yao ili kukuza ushirikiano baina yao.

 

Akizungumzia juu ya mradi wa uzalishaji hewa tiba ya oksijeni unaotarajiwa kuanza kujengwa kuwa huduma za hewa tiba ni muhimu kwa sababu ya uwepo wa mahitaji ya huduma hizo kwenye sekta ya afya hususani katika kipindi cha magonjwa ya mlipuko ambayo mengi yanahusisha masuala ya upumuaji, ajali na huduma za vyumba maalum vya watoto njiti na watoto wagonjwa.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Path Bw. Amos Mugisha amesema mradi huu ulianza mwaka 2021 na umegharimu zaidi ya Milioni 163.5 ambapo wameweza kufanya ukarabati wa jengo na ununuzi wa vifaa vya kiteknolojia vya kufundishia.

 

Aidha, ameishukuru Wizara ya Afya kwa kupata ushirikiano mzuri katika idara zote za wizara na taasisi zake na kuahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha sekta ya Afya nchi ili kutoa huduma bora kwa jamii.