Customer Feedback Centre

Ministry of Health

BOHARI YA DAWA YAUNGWA MKONO NA KAMATI YA BUNGE YA BAJETI

Posted on: April 30th, 2024

Na WAF - Dodoma

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti Mhe. Oran Njeza ameahidi kupitia Kamati yake kuiunga mkono Wizara ya Afya kupitia Bohari ya Dawa (MSD) kwa kujenga maghala na viwanda vya dawa ili kupunguza gharama za kuagiza dawa hizo kutoka nje ya nchi.

Mhe. Njeza amesema hayo jioni ya leo Aprili 30, 2024 wakati wa kikao cha kamati ya Bunge ya Bajeti baada ya wasilisho la mpango kazi wa Bohari ya Dawa (MSD) kuhusu ujenzi wa viwanda vya dawa na maghala ya kuhifadhia dawa.

“Tunaipongeza sana Wizara ya Afya, tunaiunga mkono MSD kwa kuwa ni azimio la Bunge ili kurahisisha upatikanaji wa bidhaa hizo za dawa kwa wananchi.” Amesema Mhe. Njeza

Aidha, Wabunge hao wamempongeza Waziri Ummy kwa kuwa anasema na anatenda kwa yale anayoyaahidi pamoja na kuishauri MSD kufanya utafiti wa dawa chache ambazo ni muhimu na zitajitaji ndio ziagizwe nje ili kupunguza uwgizwaji wa dawa hizo nje ya nchi na kuweka nguvu katika kutumia Tiba Lishe.

Kwa upande wake Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatoa asilimia 50 ya fedha za Dawa kwa MSD ambapo kwa leo imepokea kiasi cha Bilioni 100 kwa ajili ya kulipa deni la MSD ambalo Wizara ya Afya na Wizara ya Fedha zimekunaliana kubadilishwa na kuwa kama mtaji.

Waziri Ummy amesema, miongoni mwa hatua zitakazo chukuliwa kwa Bohari ya Dawa ni pamoja na kubadilisha muundo wa MSD ambapo Mkurugenzi Mkuu atashuhulika na masuala ya kununua na kutunza bidhaa za dawa na mengine watawaachia Sekta binafsi pamoja na kuzipa kipaumbele dawa za asili kwa maana magonjwa mengine unapona bila kutumia dawa za ‘antibiotics’.

Nae, Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Bw. Mavere Tukai wakati akiwasilisha mpango kazi huo amesema hadi kufikia Machi 30, 2024, MSD ilikuwa na mita za mraba 36,254 na mahitaji ya ziada yakiwa ni mita za mraba 63,746.

“Katika kuhakikisha Bohari ya Dawa inafanikisha majukumu yake ya msingi, tunapendekeza Bohari ya Dawa isaidiwe kwa kupewa vyanzo vitakavyowezesha kupata mkopo wenye masharti nafuu (concessional loan) utakaosaidia ujenzi wa maghala.” Amesema Bw. Mavere