Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

ZAIDI YA WASICHANA MILIONI NNE WENYE MIAKA 9-14 KUFIKIWA NA CHANJO YA HPV

Posted on: April 22nd, 2024



Na WAF - Mwanza

Serikali kupitia Wizara ya Afya imepanga hadi kufikia Disemba 2024 iwe imewafikia wasichana Milioni 4,841,298 wenye umri wa Miaka 9-14 kwa kuwapa dozi moja ya chanjo ya HPV baada ya kujiridhisha kuwa chanjo hiyo haina madhara na dozi moja inatosha.

Waziri Ummy amesema hayo Aprili 22, 2024 kwenye uzinduzi wa Maadhimisho ya Dozi moja ya chanjo ya HPV kwa wasichana wenye umri wa miaka 9 hadi 14 iliyozinguliwa katika viwanja vya Furahisha Wilayani Ilemela Mkoa wa Mwanza.

“Tutapita nyumba kwa nyumba, kitongoji, mtaa kwa mtaa, mjini, vijijini, kata kwa kata kwa kufikia lengo hili ili wasichana hawa waweze kupata chanjo ya HPV kwa lengo la kuwalinda na Saratani ya Mlango wa Kizazi”. Amesema Waziri Ummy

Waziri Ummu amewapongeza Wakuu wa Mikoa kwa kupokea jambo hilo vizuri ambapo kwa kila Mkuu wa Mkoa amekuja na takwimu zake za kufikia idadi ya wasichana ambao watakuwa wamepata chanjo hiyo ya HPV.

“Tunakwenda kuijenga Tanzania isiyo na wagonjwa wa Saratani ya Mlango wa Kizazi, kuanzia Mikoa 10, 15, 30 inayokuja, hii ndio Tanzania ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa na Watanzania wenye Afya bora ili waweze kushiriki kwenye ujenzi wa familia zao na Jamii yetu kwa ujumla”. Amesema Waziri Ummy

Aidha, Waziri Ummy ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao kupata chanjo hiyo maana kuwaficha ni kumnyima haki yake ya msingi ya kuwa na Afya bora.

“Lengo letu tunataka kufikia 90% inapofika Mwaka 2030 kwa Binti yoyote anapofikia umri wa miaka 14 awe amepata chanjo ya HPV na kuhakikisha tunafanya uchunguzi wa mapema dhidi ya Saratani ya Mlango wa Kizazi kwa kufikia 70%”. Amesema Waziri Ummy

Waziri Ummy ametoa wito kwa wanawake wote hususan wenye umri miaka 25-49 kufanya uchunguzi wa Saratani ya Mlango wa Kizazi angalau mara moja kwa mwaka kwa kuwa ugonjwa huo unapona iwapo utagundulika mapema.

“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuwezesha, tumepeleka vifaa vya kupima na kutibu mabadiliko ya awali ya Saratani ya Mlango wa Kizazi mpaka ngazi ya Zahanati, hii ni hatua kubwa kwa Tanzania”. Amesema Waziri Ummy