WIZARA YA AFYA YAZINDUA KAMATI YA WATAALAM WA UKUNGA, KUIMARISHA HUDUMA ZA AFYA YA UZAZI
Posted on: July 23rd, 2026Na Aisha Swahibu, WAF - Dar es Salaam
Wizara ya Afya imezindua rasmi Kamati ya Wataalam ya Ukunga (Midwifery Sub-Technical Working Group) kwa lengo la kuimarisha huduma za ukunga nchini na kuongeza mchango wa wakunga katika kuboresha afya ya uzazi, mama na mtoto.
Akizungumza Leo Julai 23, 2026 Jijini Dar es salaam wakati wa uzinduzi huo Mkurugenzi wa Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto Dkt. Ahmad Makuwani, amesema kuwa kuanzishwa kwa kamati hiyo kunaonesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha mifumo ya afya kwa kuwapa wataalamu wa ukunga nafasi ya kushiriki katika kupanga, kushauri na kusimamia utekelezaji wa afua za afya ya uzazi.
Ameeleza kuwa licha ya mafanikio yaliyopatikana katika kupunguza vifo vya akina mama na watoto, bado zipo changamoto ikiwemo uhaba wa wakunga wenye ujuzi maalum, tofauti za ubora wa huduma na hitaji la kuimarisha elimu pamoja na mafunzo ya ukunga.
“Kamati hii itakuwa na jukumu la kuishauri Wizara ya Afya kuhusu sera, mikakati na miongozo ya huduma za ukunga, kufuatilia utekelezaji wa afua, kuimarisha ushirikiano wa wadau na kukuza matumizi ya ushahidi wa kisayansi katika kuboresha huduma,” amesema Dkt. Makuwani.
Aidha, amebainisha kuwa uwekezaji katika taaluma ya ukunga ni miongoni mwa mikakati yenye matokeo makubwa katika kupunguza vifo vya akina mama na watoto, huku kamati hiyo inatarajiwa kutetea maendeleo ya rasilimali watu na ubora wa elimu ya ukunga nchini.
Dkt. Makuwani ametoa wito kwa wajumbe wa kamati hiyo na wadau wote kushirikiana kwa uwajibikaji ili kuimarisha huduma za ukunga nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga Bi. Ziada Sellah amesema kuanzishwa kwa kamati hiyo ni matokeo ya jitihada za muda mrefu za Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali waliotambua umuhimu wa kuwa na jukwaa la kitaalam litakaloratibu na kuimarisha maendeleo ya huduma za ukunga nchini.