Wizara Ya Afya

WIZARA YA AFYA, UDOM KUONGOZA JUHUDI ZA KITAIFA KUIMARISHA HUDUMA ZA AFYA KUPITIA POCUS NA AKILI UNDE

Posted on: April 25th, 2026

Na. WAF - Dar es Salaam

Serikali kupitia Wizara ya Afya na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya afya nchini, imeendelea kuratibu kikao maalum cha kitaifa cha wataalamu wa radiolojia na tiba ya mionzi kwa lengo la kuimarisha huduma za uchunguzi wa magonjwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

Akizungumzia hilo Aprili 24, 2026 jijini Dar es Salaam Dkt. Gerald Mrema, Mtaalamu wa Radiografia kutoka Wizara ya Afya na mratibu wa huduma za uchunguzi na tiba ameipongeza UDOM kwa ubunifu huo pamoja na juhudi zake katika kuendeleza tafiti zenye tija.

Dkt. Mrema amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Vyuo Vikuu, Serikali na Taasisi za Afya ili kukuza utafiti, kujenga uwezo wa wataalamu, na kuimarisha mfumo wa afya unaojibu mahitaji ya sasa na ya baadaye.

Akichangia mada wakati wa kikao hicho, mwakilishi kutoka UDOM, Dkt. Sophia Gibore, Mhadhiri Mwandamizi kutoka Shule Kuu ya Uuguzi na Afya ya Jamii (SoNPH), amesema kuwa hatua hiyo imechochewa na utekelezaji wa Mradi wa SAFARI, unaolenga kupanua upatikanaji wa huduma za uchunguzi wa mapema, hususan kwa wanawake katika vituo vya afya vya ngazi ya msingi.

Amesema kuwa matumizi ya teknolojia ya akili unde katika uchunguzi wa ultrasound yataongeza uwezo wa kugundua changamoto za kiafya kwa wakati, kuboresha ubora wa matibabu, na kuchangia kupunguza vifo vya mama na mtoto ikiwa ni miongoni mwa vipaumbele vya afya vya Taifa.

Kikao hicho kimelenga kuunda Kikundi Kazi pamoja na kuandaa hadidu za rejea zitakazoongoza utekelezaji wa mradi wa huduma za uchunguzi wa papo kwa papo (Point of Care Ultrasound, POCUS) kwa kutumia akili unde (AI).

Washiriki katika kikao hicho wameeleza kuridhishwa na hatua hiyo, wakitambua mchango wa Mradi wa SAFARI katika kuleta jukwaa muhimu la majadiliano ya kitaifa.

Wamebainisha kuwa teknolojia ya POCUS ina uwezo mkubwa wa kuboresha utoaji wa huduma za afya, hususan katika maeneo yenye upungufu wa wataalamu bingwa.