Wizara Ya Afya

WITO WATOLEWA KUTUMIA TEKNOLOJIA BUNIFU KUIMARISHA UBORA WA HUDUMA ZA AFYA

Posted on: October 20th, 2026

Na Aisha Swahibu, WAF – Dodoma

Wito umetolewa kwa Wizara ya Afya na Taasisi, na mabaraza yote yaliyo chini yake kutumia mifumo ya kidijitali na teknolojia bunifu kuboresha ubora wa huduma za afya, kukusanya maoni ya wananchi na kuimarisha uwajibikaji kwa watoa huduma nchini.

Akizungumza katika kikao cha Kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt. Zeyana Hamid, leo Oktoba 20, 2026, Bungeni, jijini Dodoma, amesisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa ufanisi zaidi kwa kutumia mifumo iliyopo, badala ya kutegemea ongezeko la uwekezaji pekee, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma zenye ubora unaostahili.

Amesema pamoja na uwekezaji mkubwa unaofanywa katika sekta ya afya, bado kuna haja ya kuimarisha mifumo ya kufuatilia ubora wa huduma na kuhakikisha mapungufu yanayojitokeza yanabainika na kufanyiwa kazi kwa wakati.

Aidha, Dkt. Zeyana ameeleza umuhimu wa kuimarisha uelewa wa wananchi kuhusu majukumu ya madaktari, mazingira wanayofanyia kazi na maslahi yao, huku akisisitiza kuwa juhudi hizo zinapaswa kwenda sambamba na uwajibikaji wa watoa huduma na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Amesema idadi ndogo ya malalamiko yanayowasilishwa kwenye mifumo rasmi haiwezi kutafsiriwa moja kwa moja kuwa wananchi wanapata huduma bora, kwani baadhi yao hukosa njia rahisi za kuwasilisha malalamiko au hukata tamaa ya kufuatilia changamoto wanazokutana nazo.

Dkt. Zeyana amependekeza matumizi ya tafiti za maoni ya wateja (healthcare surveys) na mifumo ya kidijitali itakayowawezesha wananchi kutoa mrejesho kuhusu huduma walizopata, huku taarifa zao zikilindwa kwa kuzingatia usiri.

Amesema kuwa,taarifa hizo zinaweza kuchambuliwa kwa kutumia teknolojia ya akili unde (AI) ili kubaini changamoto zinazojirudia na kusaidia kupanga mikakati ya kuboresha utoaji wa huduma za afya.

Amesisitiza kuwa matumizi ya mifumo hiyo yanapaswa kwenda sambamba na utekelezaji wa sheria na taratibu zilizopo za uwajibikaji, ili kuhakikisha changamoto zinazobainika zinapatiwa ufumbuzi na wananchi wanapata huduma bora, salama na zenye usawa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.