WAZIRI WA AFYA AITAKA BODI YA TMDA KUIMARISHA USIMAMIZI WA KIMKAKATI NA UWAJIBIKAJI
Posted on: October 19th, 2026Na Happyness Hans, WAF - Dodoma
Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, ameitaka Bodi ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kuimarisha usimamizi wa kimkakati na ufanisi wa utendaji wa Mamlaka hiyo ili kuhakikisha inatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia vipaumbele vya Taifa na mahitaji ya sekta ya afya.
Akizungumza leo Oktoba 19, 2026 Jijini Dodoma katika Uzinduzi wa Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa TMDA, Mchengerwa amesisitiza kuwa jukumu kuu la Bodi ni kumshauri Waziri mwenye dhamana ya afya kuhusu masuala ya kimkakati na kiutendaji yanayohusu TMDA, huku akieleza umuhimu wa kuhakikisha mipango na shughuli za Mamlaka zinaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 pamoja na agenda ya kuendeleza viwanda vya dawa nchini.
Ameeleza kuwa Bodi ina wajibu wa kuongoza uandaaji wa Mpango Mkakati wa TMDA, kuweka vipaumbele vya utekelezaji na kuidhinisha Mipango Kazi pamoja na Bajeti za mwaka ili kuhakikisha rasilimali za Mamlaka zinatumika kwa ufanisi na kuleta matokeo yaliyokusudiwa.
Aidha, ameitaka Bodi kufuatilia na kutathmini utendaji wa TMDA kupitia taarifa za utekelezaji za robo mwaka, nusu mwaka na mwaka mzima, na kuhakikisha taarifa hizo zinawasilishwa kwa Waziri kupitia Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, pamoja na Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Ofisi ya Msajili wa Hazina, kwa mujibu wa taratibu husika.
Katika kusimamia matumizi ya fedha za umma, Mchengerwa amesisitiza umuhimu wa Bodi kuhakiki hesabu za TMDA kwa kuzingatia taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali pamoja na wakaguzi wengine wanaotambuliwa kisheria.
Vilevile, amebainisha kuwa Bodi ina wajibu wa kuisimamia Menejimenti ya TMDA katika masuala yanayohusu ustawi na maslahi ya watumishi, yakiwemo mishahara, posho na marupurupu, akisisitiza kuwa rasilimali watu ndiyo msingi muhimu wa mafanikio ya taasisi hiyo.
Ameongeza kuwa usimamizi madhubuti wa kimkakati na kuzingatia ustawi wa watumishi ni nguzo muhimu katika kuimarisha utendaji wa TMDA na kuongeza mchango wake katika maendeleo ya sekta ya afya nchini.