Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WAZIRI UMMY MWALIMU AWATEMBELEA WATOTO REHEMA NA NEEMA HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI

Posted on: July 5th, 2022

Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu amewatembelea Watoto Mapacha Rehema na Neema waliofanyiwa upasuaji wa kutenganishwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Waziri Ummy amefurahishwa na hali za maendeleo ya kiafya ya Watoto hao kuendelea vizuri na kuwapongeza jopo la Madaktari kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili pamoja na Madaktari kutoka Nchi ya Falme ya Bahrain.

“Wataalamu wetu wamefanya upasuaji wa kuwatenganisha kwa mafanikio makubwa, nimefurahi kuona Watoto wanaendela vizuri, wamenieleza upasuaji huu ni mgumu sana, leo ni siku ya nne na Watoto wanaendelea vizuri tunamshukuru Mungu” amesema Waziri Ummy Mwalimu

Waziri Ummy Mwalimu amesema katika Mwaka huu mpya wa Bajeti 2022/23 Serikali imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 8 kwa ajili ya mafunzo kwa madaktari ili waweze kuongeza ujuzi na kuweza kutoa huduma za kibingwa hapa nchini.

“Tunao wajibu wa kuweka rasimali fedha kwa ajili ya mafunzo kwa watumishi, vifaatiba pamoja na dawa na miundombinu, tutaendelea kuweka fedha kwa ajili ya mafunzo kwa madaktari bingwa na bingwa bobezi” amesema Waziri Ummy

Waziri Ummy Mwalimu amempongeza Mama wa mapacha Rehema na Neema kwa ujasiri na kuweza kujifunga Watoto mapacha katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa huku akisema kuwa Wizara itaweka mkakati endelevu wa kuwafuatilia Watoto hao kujua hali zao pamoja na kutoa msaada kwa familia.