Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WAZIRI UMMY MWALIMU AWAKARIBISHA WAWEKEZAJI KUTOKA INDIA NA FALME ZA KIARABU KUWEKEZA KWENYE SEKTA YA AFYA NCHINI

Posted on: August 17th, 2022



Na Englibert Kayombo WAF, Dar Es Salaam.

Waziri wa Afya Mhe. @UmmyMwalimu leo amekutana na kufanya mazungumzo na Wawekezaji kutoka India pamoja na Umoja wa Falme za Kiarabu (United Arab Emirates) kujadili na kuwakaribisha kwenye fursa za uwekezaji katika Sekta ya Afya nchini.

Waziri Ummy amepongeza nchi hizo kwa kuonyesha nia ya kutaka kuwekeza kwenye Sekta ya Afya na kuongeza ushirikiano katika kusaidia maendeleo ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuboresha ubora wa huduma za afya.

“Tumekuwa tukishirikiana na India kwenye mambo mengi kuhusu Sekta ya Afya, tuna madaktari wetu watanzania wanasoma masuala ya udaktari huko India, tuna wawekezaji kutoka India hapa nchini, ushirikiano huu ni mzuri na una tija kwa Serikali na Watanzania”. Amesema Waziri Ummy na kuipongeza Umoja wa Falme za Umoja wa Kiarabu kwa kuvutiwa kuwekeza kwenye Sekta ya Afya hapa nchini.

Waziri Ummy amesema kuwa kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwenye Sekta ya Afya ni ubora wa huduma, hivyo kuwakaribisha wawekezaji hao kuwekeza hapa nchini ili Watanzania na raia kutoka nchi Jirani waweze kupata huduma za kibingwa za matibabu.

Aidha, Waziri Ummy ametoa wito kwa wawekezaji hao kuweka mkazo zaidi katika fursa za uwekezaji kwenye upande wa kuboresha mifumo ya TEHAMA kwenye Sekta ya Afya nchini huku akisema kuwa bado kuna changamoto nyingi kwenye mifumo ya TEHAMA ndani ya Sekta ya Afya.

Bw. Lav Aggarwal ambaye ni Kiongozi wa wawekezaji kutoka India, amesema kuwa lengo kufika nchini ni kuboresha zaidi ushirikiano baina ya nchi husika na wanatarajia kuendela kushirikiana na Tanzania katika kuboresha zaidi upatikanaji wa huduma bora za matibabu hapa nchini.

Naye Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu hapa nchini Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu hapa nchini Bw. Khalifa Al Marzooqi amesema ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mhe. Samia Suluhu Hassan katika Umoja wa Falme za Kiarabu imefungua zaidi milango ya uwekezaji kutoka Falme za Kiarabu na kufika hapa kuja kuona nini cha kuwekeza kwenye Sekta ya Afya.