Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WAZIRI MKUU MAJALIWA AWAASA MADAKTARI KUDUMISHA WELEDI, KUPINGA RUSHWA

Posted on: June 18th, 2025

Na, WAF-Arusha 


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, amekitaka Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kuendelea kusimamia weledi wa taaluma ya udaktari pamoja na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya ili kufikia malengo ya Serikali katika kuboresha huduma hizo nchini.


Mhe. Majaliwa ametoa kauli hiyo Juni 18, 2025, wakati wa akifungua Mkutano Mkuu wa Chama cha Madaktari Tanzania uliofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa AICC, jijini Arusha. Ameeleza kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa wa madaktari katika jamii na hivyo ni muhimu chama hicho kikaendelea kuwa daraja la kuhakikisha viwango vya kitaaluma vinazingatiwa kwa maslahi ya taifa.


“Ni muhimu kwa chama hiki kuendelea kuhimiza weledi na maadili kwa wanachama wake. Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kazi, lakini pia tunahitaji kuona huduma bora na za heshima kwa wananchi,” amesema Waziri Mkuu.


Aidha, Mhe. Majaliwa amewataka madaktari kutumia mkutano huo kama jukwaa la wazi kuelezea changamoto na kutoa mapendekezo ya namna bora ya kuimarisha huduma za afya, huku akisisitiza kuwa Serikali iko tayari kupokea mawazo ya wataalam hao ili kuboresha mfumo wa afya nchini.


Waziri Mkuu pia ametoa onyo kwa baadhi ya madaktari wanaokiuka maadili ya kazi kwa vitendo vya rushwa na uporaji wa vifaa tiba, akisisitiza kuwa Serikali haitavumilia watumishi wa aina hiyo.


“Ni vema kila mmoja akawa mlinzi wa taaluma hii. Tuendelee kuongeza umakini katika kazi zetu, lakini pia tudhibiti wachache wanaoichafua taswira ya taaluma hii kwa vitendo visivyofaa,” ameongeza.


Amesema Serikali imeongeza uwezo wa madaktari kwa kuwaajiri zaidi, kuwajengea uwezo, na kuboresha upatikanaji wa vifaa tiba, dawa na huduma muhimu katika vituo vya afya ili kusogeza huduma karibu na wananchi.


Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amesema madaktari wamekuwa ni nguzo muhimu katika mafanikio ya sekta ya afya nchini kwa kutoa huduma bora, zenye ubora na kwa kuzingatia utu wa mgonjwa.


“Mafanikio yaliyopo leo kwenye sekta ya afya ni kwa sababu ya madaktari wetu walioko kwenye kila ngazi ya utoaji huduma, kuanzia zahanati hadi hospitali za rufaa. Wanafanya kazi kwa kujitolea, kwa uadilifu na uzalendo mkubwa,” alisema Dkt. Mollel.


Mkutano huo wa MAT umewakutanisha mamia ya madaktari kutoka maeneo mbalimbali nchini, ukiwa na lengo la kujadili maendeleo ya taaluma hiyo, changamoto zilizopo na kutoa mapendekezo ya kisera kwa Serikali.