Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WAWEKEZAJI SEKTA YA AFYA WASISUMBULIWE" DKT MOLLEL

Posted on: March 27th, 2024

"

Na WAF, DODOMA


Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amewataka waganga wafawidhi nchini na Watumishi ndani ya Sekta ya Afya kutokuwa kikwazo kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika sekta hiyo ikiwemo uanzishaji wa vituo binafsi vya kutolea huduma za afya. 


Pia amesema sekta binafsi imesaidia kwa kiwango kikubwa kuipunguzia Serikali mzigo hasa upande wa ajira kwani vijana wengi wameajiriwa kupitia sekta binafsi, hali ambayo sio rahisi kuiachia mzigo serikali pekee.


Dtk. Mollel ameyasema hayo Machi 27,2024 wakati akifunga Mkutano wa Kwanza wa Kimataifa wa Afya ya Msingi uliofanyika Jijini Dodoma kwa muda wa siku Tatu ambapo washiriki kutoka ndani na nje ya nchi wameshiriki na kuchangia mada zilizowasilishwa wakati wa mkutano huo.


Dkt. Mollel amewaasa Wakurugenzi wa OR- TAMISEMI na Wizara ya Afya kuangalia idadi ya Vijiji ambavyo havina Zahanati ili kuhakikisha vinapata vituo hivyo mapema iwezekanavyo.


“Tukijipanga kwa muda wa miaka miwili tukapunguza semina na makongamano na tukapunguza mambo mengine, tukapunguza kidogo kuboresha huku juu zaidi kwasababu huku tunaweza kwenda kwa pamoja, nawahakikishia kwa kipindi cha miaka miwili hakuna Kijiji kitakosa Zahanati”, amesema Mollel na kuongeza .


“Tunataka tutakapokutana tena katika mkutano wa mwaka 2026 tutazungumza masula mengine kama kuajiri watumishi, kuweka vifaa na kuboresha huduma zingine zinazopaswa kuongezwa” amesisitiza Mollel.


Aidha amewaomba washiriki katika mkutano huo kuwasaidia wakurugenzi ambao bado wanaleta mgawanyiko katika kazi kuhakikisha suala hilo wanalimaliza na kuimarisha utendaji zaidi.


“Sekta ya Afya ni moja na kazi nyingi za afya zinaanzia katika ngazi ya msingi na dada yangu Dkt. Grace amesisitiza hapa hakuna huduma za afya bila msingi kwani huduma zote zinaanzia huko kwa wananchi walio wengi ndipo wanaanzia kabla ya kuja huku juu kupatiwa huduma,” amesema.


Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt.Grace Magembe amesema, ili kufanikiwa katika sekta ya Afya ni lazima kuboresha sekta kuanzia ngazi ya msingi na ustawi wa Jamii


"Hakuna Afya, bila kuhakikisha tunaboresha eneo la Afya ya Msingi na ustawi wa Jamii lipo sawa, mafaniko yetu tutaweza kujipima vizuri endapo tutatoa kipaumbele katika eneo la afya ya msingi," ameeleza Dkt. Magembe


Akitoa salaam za Ofisi ya Rais TAMISEMI, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia Afya Dkt. Charles Mahela, amesema kuwa kupitia mkutano huo mapendekezo kadhaa yameweza kutolewa kupitia majadiliano yaliyofanyika ikiwemo kuhakikisha upatikanaji wa fedha za kutosha kwa huduma za afya ya msingi.


“Mapendekezo hayo ni pamoja na kuongeza bajeti za afya za mifumo ya bima na jambo hili limesisitizwa kwa ukubwa na wakashauri vyanzo mbalimbali viweze kutumika ikiwemo kuwashirikisha wadau kama Wizara ya Fedha,”amesema.


Amesema pendekezo lingine lililotolewa ni kwa wadau pamoja na Serikali kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya afya ya msingi, rasilimali watu na vifaa ili kuendelea kuboresha upatikanaji wa huduma bora.


MWISHO