Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WATUMISHI WAASWA KUSHIRIKI KUREJESHA KWA JAMII ZENYE UHITAJI.

Posted on: February 24th, 2025

Na WAF - Dodoma.

Waandishi waendesha Ofisi wakishirkiana na watumishi wa kada zingine kutoka Wizara ya Afya wametoa wito kwa watumishi wa umma na jamii kwa ujumla kujiwekea utaratibu wa kurejesha kwa jamii zenye uhitaji badala ya kuiachia Serikali pekee.

Hayo yamebainishwa Februari 22, 2024 na Muandishi Muendesha Ofisi Mkuu Bi. Eugenia Rimoy wakati Wandishi waendesha Ofisi wakishirikiana na watumishi kada zingine kutoka Wizara ya Afya walipokwenda kuwatembelea na kutoa Misaada kwa watoto waishio katika kituo cha kulelea watoto wenye uhitaji, Kikombo, Jijini Dodoma.

Bi. Rimoy amesema kila mmoja katika jamii anatakiwa awe sababu ya kumpa furaha mwenzake hususani makundi yenye uhitaji maalum ili kuwafariji na kuwapa tabasamu.

“Katika maisha tunayoishi tunatakiwa kuwabariki wengine ambao wana mahitaji, kwa hiyo tuisihi jamii iweze kutafakari na kutambua kama Mungu amekubariki kupata kitu unapaswa kuwapatia na wengine pia ili kuwapa tabasamu wahitaji,” amesema Bi. Rimoy.

Bi. Rimoy meongeza kuwa kwa kuanzia wameanza kwa kukabidhi vitu mbalimbali vyenye thamani ya Shilingi Millioni 3 ambapo lengo ni kuifikia jamii kwa upana zaidi na vituo vingine pia.

Akizungumza kwa niaba ya Mfawidhi wa Makao ya Kikombo, Afisa Ustawi wa Jamii Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo Bw. Arnold Fyataga amesema, Makao hayo yalizinduliwa Juni 16, 2021 na Makamu wa Rais Mh Dkt. Philip Mpango na Kituo kilianza kuhudumia watoto 28 na kwa sasa kituo kina watoto 185, watumishi 27 na wanaojitolea ni 4.

“Tunashukuru sana kwa kuja, asanteni sana kwa zawadi mlizotuletea Mwenyezi Mungu awabariki na kuwazidishia kwa ukarimu wenu. Tumefurahia zawadi mlizozitoa na tumezipokea kwa furaha, ” amesema Bw. Fyataga.