Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WATUMISHI WA AFYA KULIPWA STAHIKI ZAO KWA WAKATI

Posted on: September 14th, 2023

Na. WAF - Songwe 


Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dkt. Francis Michael kuwahimiza Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa huo kuwalipa watumishi wa Afya stahiki zao kwa wakati. 


Waziri Ummy ameyasema hayo Septemba 13, 2023 wakati akiongea na wajumbe wa Timu za Usimamizi na Uendeshaji wa huduma za Afya ngazi ya Mkoa (RHMT) na Halmashauri zote za Mkoa (CHMT) na Wajumbe wa Timu ya Uendeshaji wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa (RRHMT) wakati akihitimisha ziara yake katika Mkoa wa Songwe.


“Naomba sana Mhe. Mkuu wa Mkoa kupitia kwako kuwahimiza Wakurugenzi kuwalipa watumishi wa Afya stahiki zao kwa wakati ili wapate moyo wakuendelea kutoa huduma katika vituo vyetu vya Afya”. Amesema Waziri Ummy.


Waziri Ummy amesema Wakurugenzi wengine waige mfano kwa Mkurugenzi wa Momba ambaye amewagawia viwanja watumishi wa Afya hivyo, lazima kuwajengea motisha na kuwavutia watumishi hao wa Afya ili waendelee kufanya kazi katika Halmashauri za Mikoa.


Aidha, Waziri Ummy wakati akihitimisha ziara yake amesisitiza kuwa, Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejenga vituo vya Afya kutoka 167 hadi 254, hivyo kwa sasa wananchi wanadai huduma bora. 


“Tumetoka kwenye vituo vya Afya 167 mpaka 254 kwa hiyo nachotaka kukisisitiza, tumejenga sana, sasa wananchi hawatudai tena majengo bali wanadai huduma bora, upatikanaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba”. Amesema Waziri Ummy.


Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dkt. Francis Michael amemuomba Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu kupeleka watumishi wa Afya hasa madaktari Bingwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo. 


“Hili ni jambo kubwa sana Mhe. Waziri tunakuomba sana utuletee madaktari bingwa katika Mkoa wetu, haya mengine ya fedha Mhe. Rais ametuletea fedha nyingi na bado anaendelea kuleta ili kuendelea kuboresha upatikanaji wa huduma bora za Afya kwa wananchi”. Amesema Dkt. Michael