Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WATUMISHI MAABARA YA TAIFA YA AFYA YA JAMII WATAKIWA KUZINGATIA MAADILI KATIKA UTENDAJI

Posted on: June 20th, 2025

Watumishi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii wametakiwa kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao ya kila siku kwa weledi na ubora unaotakiwa kwa  kuzingatia maadili ya utendaji kazi kwa kada zao kwa mujibu  wa Kanuni za utumishi wa umma za mwaka 2005 (public service code of ethics and conduct),ili kuleta tija.


Wito huo umetolewa leo Juni 20, 2025  Jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii Bw. Ambele Mwafulango wakati akifunga semina elekezi ya siku moja kwa watumishi wa Maabara ya Taifa uliyolenga kutoa elimu ya Utawala Bora katika Utumishi wa Umma,  Mapambano dhidi ya Rushwa mahala pa kazi, mafao yatokanayo na Mfuko wa PSSSF na taratibu za kufuatilia michango ya mwanachama na dhana ya Uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma (Haki na Wajibu)


Awali akiwasilisha mada katika semina hiyo, Afisa Uchunguzi Mwandamizi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wakili Msomi Bi. Janet Kafuko amesisitiza kuhusu umuhimu wa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma  na uwajibikaji kwakuwa ni mambo ya kisera na kisheria ambayo yana misingi muhimu nane (8)  ya kutoa huduma bora kwa kuzingatia utalaam/weledi, utii kwa Serikali, nidhamu na bidii ya kazi, kutoa huduma bila upendeleo, kufanya kazi kwa uadilifu, Kuwajibika kwa umma, kuheshimu sheria na matumizi sahihi ya taarifa.


 Bi. Kafuko ameelezea faida za kuzingatia maadili katika utumishi wa umma, athari za ukiukwaji wa maadili, njia za kudhibiti ukiukwaji wa maadili na adhabu kwa mtumishi aliyekiuka maadili ya utumishi wa umma.


Akiwasilisha mada ya kupambana na Rushwa Bi  Kafuko ameelezea wajibu wa Serikali kwa wananchi wa Tanzania, hali ya rushwa nchini, Madhara ya rushwa nchini na wajibu wa watumishi wa Maabara ya Taifa kwenye vita dhidi ya rushwa na kuielezea  sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa Na.11/2007 na Makosa ya rushwa. 


Awali akiwakaribisha watumishi wa Maabara ya Taifa Afisa Rasilimali watu Maabara ya Taifa Bw. Athuman Masesa aliwataka watumishi kuhakikisha wanasikiliza na kuelewa mafunzo hayo muhimu kwa ustawi wa utumishi wao wa Umma na kuhakikisha watakayojifunza wanakwenda kuyatendea kazi.