Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WATOTO MILIONI 9.4 WAPATIWA DOZI MBILI ZA VITAMINI A 2024.

Posted on: July 20th, 2025

Na. WAF, Dar es Salaam


Serikali kupitia Wizara ya Afya imefanikiwa kufikia zaidi ya asilimia 90 ya ufanisi katika utoaji wa Vitamin A kwa watoto wenye umri wa miezi 6 hadi 59 ambapo watoto milioni 9.4 sawa na asilimia 97 ya watoto waliopokea dozi mbili za Vitamin A wamefikiwa kwa mwaka 2024 .


Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Dkt. Otilia Gowelle akimwakilisha Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama katika ziara ya kikazi ya ufuatiliaji wa Huduma za utoaji wa Vitamini A wakati wa mwezi wa Afya na lishe kwa watoto, Juni 19, 2025 katika zahanati ya kijitonyama, jijini Dar es Salaam.


Amesema kwa mwaka 2025 lengo la Serikali ni kuwafikia watoto takribani milioni 9.5 kwa dozi hizo mbili za lazima za Vitamin A.


“Wizara inatambua umuhimu wa huduma zinazotolewa wakati wa Mwezi wa Afya na Lishe kwa Watoto (CHNM) kama moja ya nguzo kuu katika mkakati wetu wa kitaifa wa afya ya mtoto. Kampeni hii inahakikisha kuwa watoto chini ya umri wa miaka mitano wanapatiwa vitamin A, dawa za minyoo, na wanachunguzwa ili kubaini utapiamlo, katika vituo vya afya na huduma za mkononi,” amesema Dkt. Gowelle.


Dkt. Gowelle amesema Ili kuhakikisha hakuna mtoto anayebaki nyuma, ni muhimu kuanza kuunganisha utoaji wa Vitamin A na huduma nyingine muhimu za afya na lishe hivyo Serikali itashirikiana na washirika kama Nutrition International kufanya majaribio hayo.


Aidha Dkt. Gowelle ameipongeza na kuishukuru Serikali ya canada na Shirika la Nutrition International kwa kuunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania kuhakikisha inalinda afya za watoto kwa kupatiwa Vitamini A ili kuwakinga na utapiamlo na vifo.


Dkt. Gowelle ametoa wito kwa washirika na wafadhili kutambua umuhimu wa Vitamin A kama njia ya kuingilia kuboresha upatikanaji na matumizi ya huduma nyingine za afya miongoni mwa jamii.


Kwa upande wake Balozi wa Canada  nchini Tanzania Mhe. Emily Burns amesema Serikali ya Canada imeahidi kuendelea kuwa mshirika wa Tanzania katika kuimarisha na kulinda afya na lishe za watoto.