Wizara Ya Afya

WATAALAMU WA MAABARA WATAKIWA KUIMARISHA USALAMA WA UTUNZAJI WA VIMELEA HATARISHI NA SAMPULI

Posted on: June 14th, 2026

Na Atley Kuni, WAF – Arusha

Wataalamu wa maabara nchini wametakiwa kuzingatia kwa umakini mkubwa maadili na viapo vya taaluma yao ili kuhakikisha jamii inalindwa dhidi ya majanga yanayoweza kusababishwa na utunzaji usio salama wa vimelea hatarishi pamoja na sampuli zinazohifadhiwa kwa muda mrefu.

Wito huo umetolewa na Mratibu wa Afya Moja kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Bi. Valentino Sanga, wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha siku tano kinachofanyika jijini Arusha kuanzia Juni 15 hadi 19, 2026.

Akizungumza katika ufunguzi huo, Bi. Sanga amesema kuwa kikao hicho kinalenga kuwajengea washiriki uwezo kupitia kubadilishana uzoefu, kukumbushana wajibu wao wa kitaaluma na kujifunza maarifa mapya yanayozingatia miongozo ya kisasa ya kitaifa na kimataifa kuhusu usalama wa maabara.

Amesisitiza kuwa wataalamu wanapaswa kutumia kikao hicho kama fursa ya kuboresha utendaji wao, hususan katika kuzuia na kubaini mapema vihatarishi vya kiafya, pamoja na kuhakikisha vimelea hatarishi na sampuli zinazohifadhiwa kwa muda mrefu zinatunzwa kwa usalama ili zisije zikawa chanzo cha madhara kwa jamii.

"Tukitumia kikao hiki vizuri, tutaweza kuimarisha mifumo ya kinga, utambuzi wa mapema wa vihatarishi na usimamizi salama wa vimelea na sampuli zinazohifadhiwa kwa muda mrefu ili kuzuia madhara kwa jamii," amesema Bi. Sanga.

Aidha, amefafanua kuwa wataalamu hao wanapaswa kuzingatia kikamilifu maadili ya taaluma yao, akibainisha kuwa uzembe katika utunzaji wa vimelea unaweza kusababisha madhara makubwa kwa wananchi na kuwa kinyume na dhamira ya kazi waliyopewa.

Pia amewahimiza washiriki kuendelea kuzingatia miongozo ya kitaifa na kimataifa inayosimamia usalama wa maabara, akisisitiza kuwa Tanzania ni sehemu ya mikataba mbalimbali ya kimataifa inayolenga kulinda afya na usalama wa jamii kupitia utekelezaji wa viwango vinavyokubalika kimataifa.

Kwa upande wake, mdau wa maendeleo kutoka taasisi ya Center for International Health, Education and Biosecurity Tanzania (CIHEB-Tanzania), Bw. Samwel Mulungu, amesema taasisi hiyo kupitia Mradi wa Usalama wa Afya Duniani