Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WATAALAM WA OPTOMETRIA WATAKIWA KUZINGATIA MIIKO YA TAALUMA YAO

Posted on: February 14th, 2026

Na WAF, Dodoma

Wataalamu wa wa Opmetria waliohitimu masomo yao na kusajiliwa na Baraza la Optometria kutoka Wizara ya Afya wametakiwa kufanya kazi kwa weledi kulingana na taratibu na kanuni za taaluma yao ili kuweza kuhudumia wananchi kwa ufasaha.

Wito huo umetolewa February 12, 2026 jijini Dodoma na Mkurugenzi msaidizi wa Rasilimali Watu na Utawala Bi. Monica Andrew wakati akifunga mafunzo yaliyoandaliwa na Baraza hilo ili kuwejengea uwezo wataalam hao kabla ya kwenda kwenye vituo vya kazi watakavyoenda kutoa huduma.

Bi Monica amesema utumishi wowote bila nidhamu kazini ni sawa na kutembea bila kuwa na uelekeo hali itakayofanya kutumbukia shimoni au kufika eneo ambalo halijakusudiwa, hivyo amewataka wataalam hao kuheshimu muda na nafasi waliyonayo.

“Ninawaomba sana nafasi mtakazopata za ajira huko mnapoenda zingatieni nidhamu kazini, wananchi wana matumaini makubwa ya kupata huduma kutoka kwa wataalam kama nyinyi, hivyo ni jukumu la kila mmoja wenu kuhakikisha anaitendea haki taaluma yake”, amesema Bi. Monica.

Aidha, Bi. Monica amewaasa wataalam hao wa Optometria kuhakikisha wanashirikiana na wataalam wa kada nyingine ili kufikia azimio la kutoa huduma bora kwa wananchi kama ilivyo dhamira ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ya huduma bora za afya kwa wananchi wote.

Naye Msajili wa Baraza hilo Bw. Sebastiano G. Millanzi amesema Baraza hilo litaendelea kusimamia weledi kwa wataalam wa Optometria ikiwa ni pamoja na kuwajengea uelewa wa taaluma hiyo lengo likiwa ni kuwafanya waweze kutimiza wajibu wao wakiwa kazini na kutoa huduma bora kwa jamii.

Mafunzo hayo yalihitimishwa na utoaji wa vyeti ambapo jumla ya wataalam 38 walipewa Vyeti vya Usajili wa Kudumu na Leseni, na wataalam 28 walipewa vyeti vya Usajili wa Awali ambavyo vinawafanya kutambulika na Baraza hilo.