WATAALAM WA AFYA WATAKIWA KUZIPA KIPAUMBELE HUDUMA ZA CHANJO ZA MKOBA
Posted on: June 12th, 2025
Na WAF - MOROGORO.
Waganga Wakuu wa mikoa, wataalam na wadau wa sekta afya wametakiwa kuongeza juhudi na ubunifu ili kuhakikisha huduma za chanjo kupitia huduma za mkoba zinafikia watoto wengi zaidi katika maeneo mbalimbali hali itakayopunguza vifo vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano vitokanavyo na magonjwa ya virusi.
Hayo yamebainishwa leo Juni 11, 2025 mkoani Morogoro na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt Grace magembe ambaye pia ni Mganga Mkuu wa Serikali wakati akifungua mkutano wa mwaka wa tathmini ya huduma za chanjo nchini.
Dkt. Magembe ameeleza kuwa idadi ya watoto wanaopatiwa huduma za chanjo imefikia asilimia 95 kwa takwimu za wastani kitaifa, hivyo ni vyema ya kuwa na mikakati itakayowezesha kufikia asilimia 100.
“ Suala la huduma za Mkoba za chanjo kutoka sasa ijulikane kwamba ni kipaumbele, na ziwe zinagusa nyanja zote kwakuwa huduma zote ni sawa na zinatakiwa kutolewa kwa wote, na tutumie nafasi zote kuhakikisha tunamfikia kila mtoto,” amesema Dkt. Magembe.
Dkt. Magembe amesema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwenye Sekta ya Afya ambao kwa sasa asilimia 80 ya Watanzania wanapata huduma bora za afya ndani ya kilomita 5 za maeneo yanayowazunguka.
Amesema pia serikali inaendelea kufanya jitihada za kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto, na kuiomba jamii nayo kutilia mkazo suala la chanjo kwa watoto wa kuanzia umri wa miaka Sifuri hadi Miaka 5 ili kuwakinga vifo na maradhi watoto.
Naye Kaimu Mkurugenzi huduma za Kinga Wizara ya Afya Dkt. Otilia Gowelle amesema Serikali kwa mwaka 2024 imevuka malengo ya ufuatiliaji wa magonjwa yanayozulika kwa chanjo ya Taifa na kuzidi kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji katika minyororo ya chanjo iliyopo.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Mpango wa Taifa wa Chanjo Dkt. Georgina Joachim amesema kwa Mwaka 2024 kampeni ya chanjo ya Surua na Rubela ilifanikiwa kuwafikia walengwa milioni 10 ambayo ni sawa na asilimia 110 kwa watoto wenye miezi 9-59.