Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WAJUMBE TAC WATAKA KLABU ZA AFYA, LISHE SHULENI KUIMARISHWA

Posted on: July 20th, 2025

Na WAF, Morogoro 


Wajumbe wa Kikao cha Kamati ya Kitaalam cha Ushauri cha Mpango wa Taifa wa Huduma za Afya na Lishe Shuleni(TAC) wamependekeza  kuimarisha uratibu wa Klabu za Afya na lishe shuleni kwa kuzingatia muongozo wa  uanzishwaji na uendeshwaji wa mabaraza ya watoto.


Wakizungumza leo  Juni 21, 2025 mkoani Morogoro  katika Kikao cha Kamati ya Kitaalam cha Ushauri wa Mpango wa Taifa wa Huduma za Afya na lishe shuleni wajumbe hao wamesema uimarishaji wa Klabu hizo utasaidia kwa kiwango kikubwa kwenye utekelezaji wa afua za lishe shuleni.


Kwa mujibu wa tathmini  iliyofanyika hivi karibuni mkoani Morogoro katika shule za msingi na sekondari wilaya za Ifakara na Gairo, kila shule ina muongozo wake ambao unaandaliwa ama na wadau, shule zenyewe na hata halmashauri, hivyo kutofautiana kati ya shule mmoja na nyingine.


"Haya si maelekezo ya Wizara, hivyo tujipange ili shule ziwe na klabu ambazo maudhui yake yameidhinishwa na Serikali," amefafanua Mwenyekiti wa kikao hicho, Dkt. Otilia Gowelle.


Kikao hicho kinachoendelea mkoani Morogoro  kitatoka na maazimio yatakayowezesha kutekeleza mpango huo kwa ufanisi. 


Wizara za Kisekta zilizokutana ni Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya  Rais TAMISEMI, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wizara ya Elimu, Wizara ya Mifugo, Wizara ya Mifugo na Wizara ya Afya.