Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WAHUDUMU NGAZI YA JAMII KUINUFAISHA RUVUMA

Posted on: December 11th, 2024

Na WAF - Ruvuma

Jumla ya Vitongoji 443, Vijiji 56, Mitaa 95 vinatarajia kunufaika na Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii katika mkoa wa Ruvuma.

Hayo yamebainishwa Desemba 10, 2024 katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma na Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Ruvuma Bw. Joel Mbewa akimwakilisha Mkuu wa Mkoa huo kwenye kikao cha kutambulisha utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii mkoani hapo katika Manispaa ya Songea na Songea vijijini.

Mbewa ametoa wito kwa jamii na watumishi kuupokea mpango huo kwani una manufaa makubwa katika sekta ya afya.

"Mkoa umepewa kipaumbele ambapo jumla ya vitongoji 443 , vijiji 56 na mitaa 95 itanufaika kupitia Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii na jumla ya wahudumu wa afya ngazi ya jamii 1,076 watapatikana kupitia mpango huo,"amesema Bw. Mbewa.

Akizungumzia historia ya wahudumu ya afya katika ngazi ya jamii, Bw. Mbewa amesema ilianzia mwaka 1970 ambapo walitekeleza masuala ya elimu ya afya, lishe na ustawi wa jamii pamoja na usafi wa mazingira na kupambana na magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza.

Kwa upande wake Afisa kutoka Mpango wa Taifa wa Huduma za Afya Ngazi ya Jamii, Bw. Bahati Mwailafu amesema zoezi la kuwachagua wahudumu ngazi ya jamii litafanyika kwa kuitisha mikutano ya hadhara ili kuwa na uchaguzi huru na wa haki.

"Mikutano ya hadhara ngazi ya vitongoji na mitaa itaitishwa ili wananchi wachague mtu wanayemwamini na kutakuwa na wahudumu wa afya wawili kila mtaa au kitongoji mwanamke na mwanaume," amefafanua Bw. Mwailafu.

Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii ulizinduliwa Januari 30, 2024 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ukiwa na mikoa 10 ya kuanzia kwa awamu ya kwanza.