WADAU WA AFYA WAKAZIA UBORESHAJI WA MIFUMO YA UCHUNGUZI KATIKA KUANDAA MPANGO MKAKATI WA TAIFA WA HUDUMA ZA UCHUNGUZI 2026–2031
Posted on: June 20th, 2026Na Abduly Iddy, Dar es Salaam
Washiriki wa zoezi la kuandaa Mpango Mkakati wa Taifa wa Huduma za Uchunguzi wa Afya wa mwaka 2026–2031 wamekubaliana kuimarisha mifumo ya uchunguzi, usimamizi wa taarifa na matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuongeza ubora na ufanisi wa huduma za uchunguzi nchini.
Makubaliano hayo yamefikiwa katika siku ya nne ya kikao kazi cha kuandaa mpango huo kilichofanyika Juni 18, 2026 jijini Dar es Salaam, ambapo makundi mbalimbali yamewasilisha uchambuzi wa hali halisi (SWOT Analysis) na mapendekezo ya maboresho katika maeneo ya uongozi, rasilimali watu, tafiti na ubunifu, miundombinu, mifumo ya maabara, usambazaji wa sampuli pamoja na masuala ya ufadhili wa huduma za uchunguzi.
Wakati wa majadiliano, washiriki wamepitia nyaraka zilizowasilishwa na kutoa maoni, mapendekezo na marekebisho yaliyolenga kuboresha ubora wa mpango huo kabla ya kuwasilishwa kwa hatua zinazofuata za uhakiki na maboresho. Aidha, wamekubaliana kuwa viongozi wa makundi wakusanye maoni yote yaliyotolewa na kuyajumuisha katika nyaraka husika kabla ya kuwasilishwa tena kwa mapitio ya mwisho.
Miongoni mwa maeneo yaliyopewa kipaumbele ni pamoja na kuimarisha mifumo ya taarifa za uchunguzi, usalama wa taarifa na uhifadhi wa takwimu kwa muda mrefu. Washiriki wameeleza umuhimu wa kuwa na mifumo inayowasiliana na kushirikiana kwa ufanisi ili kuhakikisha upatikanaji wa taarifa sahihi kwa ajili ya kufanya maamuzi na kuboresha huduma kwa wananchi.
Katika eneo la rasilimali watu, washiriki wamependekeza kutenganisha masuala ya usimamizi wa rasilimali watu na maendeleo ya rasilimali watu ili kuongeza ufanisi katika upangaji, ajira, mafunzo na tathmini ya utendaji. Aidha, wamehimiza shughuli za maendeleo ya wataalamu ziende sambamba na mahitaji ya mifumo ya kisasa ya uchunguzi wa afya.