Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

VIFO VYA UZAZI VYAPUNGUA KWA ASILIMIA 18 NYANDA ZA JUU KUSINI MAGHARIBI

Posted on: December 13th, 2024

Na WAF - Mbeya

Vifo vitokanavyo na uzazi vimeendelea kupungua kwa asilimia 18 kutoka vifo 121 kwa vizazi hai 100,000 kwa mwaka 2021 hadi kufikia vifo 83 kwa vizazi hai 100,000 mwaka 2023 katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi.

Hayo yamesemwa Desemba 12, 2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya Dkt. Godlove Mbwanji wakati akifungua kikao kazi cha kufanya tathimini na kubadilishana uzoefu vya utekelezaji wa njia bora za kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na mtoto kwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi ambayo ni mikoa ya Mbeya, Songwe na Rukwa.

Dkt. Mbwanji amesema kupungua kwa vifo hivyo ni jitihada
kubwa za uwekezaji uliofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika miundombinu, vifaa na vifaa tiba vya kisasa pamoja na utendaji kazi bora wa watumishi wa sekta ya Afya nchini kwenye vituo vyote vya kutolea huduma za afya.

“Tutumie fursa hii na kutoa pongezi nyingi na shukrani kwa watumishi wa sekta ya Afya walio chini kwa kujitoa kwao kuwahudumia wananchi bila kujali changamoto wanazokutana nazo,” amesema Dkt. Mbwanji.

Aidha, ameongeza kuwa kauli mbiu ya kikao hicho ni uongozi na uwajibikaji ni chachu ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga hivyo amewataka viongozi wa hospital zote mikoa ya nyanda za juu kusini magharibi kutoa uongozi unaozingatia utu na kujali wanao waongoza.

“Ni wajibu wetu kuwa viongozi wenye kujali utu kwa watumishi wetu na wao wana wajibu wa kuwajibika kutimiza wajibu wao ili sisi sote kwa pamoja tuweze kupata matokeo mazuri zaidi,” amesema Dkt. Mbwanji

Awali akitoa salamu za Wizara ya Afya Afisa Program ya uzazi salama Dkt. Ulimbakisye Macdonald amesema kazi nzuri inafanyika ndani ya mikoa ya kupunguza vifo vya mama na mtoto ni lazima kukumbushana juu ya uwajibikaji kwenye maeneo yetu ya kazi ili kazi hizo nzuri ziendelee kuleta tija kwa taifa.