Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

UZALISHAJI WA DAWA NCHINI UTASAIDIA UPATIKANAJI WA DAWA KWA WAKATI NA GHARAMA NAFUU

Posted on: December 20th, 2023

NA: WAF, Dar es Salaam

Waziri wa afya Mhe. Ummy Mwalimu ametoa rai kwa Wadau wa Maendeleo kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kuwekeza zaidi nchini kwenye Sekta ya Afya huku wakiiga mfano wa Kampuni ya uzalishaji wa Dawa cha Cure Afya ambayo iko mbioni kuanza uzalishaji wa dawa hapa hapa nchini.

Waziri Mhe. Ummy ameyasema hayo leo Disemba 20, 2023 alipo tembelea Kiwanda kipya cha utengenezaji Dawa cha Cure Afya ambacho kipo Wilaya ya Kigamboni Jiijini Dar Es Salaam kwa ajili ya kuona utayari wa Kiwanda hicho kutengeneza Dawa kwa ajili ya soko la ndani ya nchi pamoja na nchi jirani.

“Dawa zinazozalishwa zitarahisisha upatikanaji wake kwa wakati, tofauti na tukiagiza dawa nje ya nchi zinachukua miezi 6 hadi 9 kuweza kufika hivyo inachukua muda mrefu mpaka kufika nchini”. Amesema Waziri Ummy.

Amesema serikali imejizatiti kukuza uzalishaji wa dawa wa ndani ili kupunguza gharama ya uagizaji kwani Tanzania ni miongoni mwa nchi nne za Afrika ambazo zinatambulika kwa umahiri kupitia Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba TMDA na Shirika la Afya Duniani WHO.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Cure Afya Bw. Paresh Ghelani amesema kuwa wako tayari kwa uzalishaji wa dawa kuanzia Januari 2023 ikiwa ni takwa la Serikali katika uwekezaji wa viwanda kwa mahitaji ya nchi ambayo yatakwenda kurahisisha upatikanaji wa dawa kwa wakati na gharama nafuu.

Haya ni matokeo chanya ya uhamasishaji Fursa za Uwekezaji wa Viwanda nchini yanayofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo ya Sekta ya Afya nchini katika kuendelea kuboresha Sekta ya Afya nchini na kuifanya Tanzania kuwa Kituo cha Utalii tiba ukanda wa Afrika Mashariki.