Wizara Ya Afya

UWEKEZAJI WA SEKTA YA AFYA WAONGEZA IMANI NA KUBORESHA HUDUMA TANZANIA

Posted on: April 20th, 2026

Na Aisha Swahibu, WAF - Dar es Salaam

Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema kupitia maboresho yaliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Sekta ya afya zimerejesha imani ya wananchi katika sekta ya afya

Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo leo Aprili 16, 2026 wakati akimkaribisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Pili wa Shirikisho la Jumuiya ya Madaktari bingwa wa upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu, jijini Dar es salaam, na kupongeza na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuimarisha sekta ya afya, hatua ambayo imeanza kuleta mabadiliko makubwa katika utoaji wa huduma kwa wananchi kote nchini.

Amesema kuwa kupitia uwekezaji huo, miundombinu ya afya imeboreshwa, vifaa tiba vimeongezwa, na huduma muhimu zimepanuliwa ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi.

Mhe. Mchengerwa ameeleza kuwa hatua hizo si tu zimeimarisha mifumo ya utoaji huduma, bali pia imani ya wananchi imerejea ambapo Wananchi wengi sasa wanashuhudia ongezeko la ubora wa huduma, huku vituo vya afya vikitoa huduma kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya sasa.

“Chini ya uongozi wako Mhe. Rais, sekta ya afya imepiga hatua kutoka kuwa mfumo unaolenga zaidi kutibu magonjwa hadi kuwa nguzo muhimu ya kulinda utu wa binadamu, kuimarisha familia, na kuchochea maendeleo ya taifa. Wadau wa afya wanasema mwelekeo huu unaakisi dhamira ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora bila ubaguzi” amesema Mhe. Mchegerwa

Ameongeza kwa mujibu wa tathmini za hivi karibuni, maboresho hayo yanaonekana wazi katika maeneo mbalimbali, ikiwemo ongezeko la upatikanaji wa huduma hata katika maeneo yaliyokuwa mbali, kupungua kwa changamoto za upatikanaji wa tiba, na kuongezeka kwa imani ya wananchi kwa watoa huduma za afya.