UJIO WA MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA FURSA UBORESHAJI WA HUDUMA
Posted on: May 18th, 2025
Na WAF - MBEYA.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dkt. Juma Zuberi Homera, amewapokea rasmi Madaktari Bingwa 49 waliowasili mkoani humo chini ya Mpango wa Madaktari Bingwa wa Rais Samia, unaotekelezwa na Wizara ya Afya. Madaktari hao watapangiwa kazi katika hospitali za halmashauri saba (7), ambapo kila hospitali itanufaika na huduma kutoka kwa madaktari bingwa saba.
Akizungumza katika hafla ya kuwapokea iliyofanyika tarehe 26 Mei, 2025 katika Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa, Dkt. Homera amesema ujio wa madaktari hao ni fursa muhimu katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Mkoa wa Mbeya. Aidha, ameeleza kuwa mpango huo unawawezesha pia watumishi wa sekta ya afya waliopo kuongeza ujuzi na uwezo wao wa kitaaluma kupitia mafunzo ya vitendo na kushirikiana na madaktari bingwa hao.
"Ujio wa Madaktari Bingwa wa Rais Samia katika hospitali zetu ni ishara ya dhamira ya kweli ya Serikali katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi. Ni fursa ya kipekee kwa watumishi wetu wa afya kuongeza ujuzi wao na kubadilishana uzoefu na wataalam hawa waliobobea," amesema Dkt. Homera.
Dkt. Homera pia amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa ubunifu na utekelezaji wa mpango huu unaosaidia kupunguza gharama kwa wananchi wanaolazimika kusafiri mbali kufuata huduma za kibingwa.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dkt. Elizabeth Nyema, ameipongeza Wizara ya Afya kwa kuendeleza mpango huo wenye tija, akisema umechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza rufaa zisizo za lazima kwenda hospitali za rufaa na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwenye hospitali za halmashauri.
Naye Mratibu kutoka Wizara ya Afya, Bi. Desteria Nanyanga, amesema lengo kuu la mpango huo ni kuboresha huduma za afya kwenye ngazi ya halmashauri sambamba na kuwajengea uwezo watumishi wa afya waliopo.
Amewataka madaktari bingwa kuhakikisha wanashirikiana kikamilifu na watoa huduma waliopo ili kutimiza malengo ya Serikali ya awamu ya sita, kwa manufaa ya wananchi wote.
Mpango huu wa Madaktari Bingwa wa Rais Samia umeendelea kuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi, hasa wa maeneo ya pembezoni, kwa kuwafikishia huduma bora za afya karibu na makazi yao.