Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

UDUMAVU WASHUKA KUTOKA ASILIMIA 48 HADI 30

Posted on: October 1st, 2025

Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa amesema kuwa kiwango cha udumavu miongoni mwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano nchini kimeshuka kutoka asilimia 48 mwaka 1992 hadi asilimia 30 mwaka 2022.

Amesema hayo leo Septemba 30, 2025 wakati alipofunga mkutano wa 11 wa wadau wa lishe nchini, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa APC uliopo Bunju, Jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan inatambua kuwa lishe si suala la kiafya pekee, bali ni nguzo ya maendeleo ya rasilimali watu, uchumi na jamii.

“Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na chakula cha kutosha, afya njema na lishe bora,” amesema Mhe. Majaliwa.

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete amesema kuwa Serikali itahakikisha kuwa wadau wote walioanishwa katika Mpango Jumuishi wa masuala ya Lishe wanaendela kutekeleza majukumu yao.

“Hii ni pamoja na kuhakikisha kuwa Wizara zote zinaingiza masuala ya lishe katika mipango ya kibajeti kila mwaka,” amefafanua.

Ameongeza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu imefanikiwa kukamilisha zoezi la utafiti wa gharama za utapiamlo ambao ulilenga kubainisha gharama na athari za utapiamlo katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.