Wizara Ya Afya

UBORA WA HUDUMA ZA AFYA NI KIPAUMBELE SAMBAMBA NA BIMA YA AFYA KWA WOTE- DKT.SAMIZI

Posted on: October 20th, 2026

Na Shabani Juma, WAF – Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Afya inatambua kuwa pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya afya, bado zipo changamoto zinazohitaji kufanyiwa kazi ili kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi.

Huku ikisisitiza umuhimu wa kuimarisha ubora wa huduma za afya nchini kwa kuhakikisha uwekezaji unaofanyika katika ujenzi wa vituo, upatikanaji wa watumishi, vifaa tiba na dawa unaendana na huduma bora kwa wananchi.

Hayo yameelezwa leo Oktoba 20,2026 Bungemi Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Afya Dkt.Florence Samizi mbele ya kikao cha Kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI.

Amesema ubora wa huduma za afya haupatikani kwa siku moja, bali ni mchakato unaohitaji usimamizi endelevu, ufuatiliaji wa utendaji wa watoa huduma na matumizi ya mrejesho kutoka kwa wananchi ili kubaini maeneo yanayohitaji maboresho.

Ameeleza kuwa, Serikali inaendelea kupokea maoni na mapendekezo yaliyotolewa na wajumbe wa Kamati hiyo kwa lengo la kuyafanyia kazi na kuhakikisha changamoto zinazobainishwa zinapata ufumbuzi.

Aidha, Dkt. Samizi amesema utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote unahitaji kuzingatia ubora wa huduma ili wananchi wanapopata fursa ya kutumia bima hiyo waweze kupata huduma zinazokidhi mahitaji yao. Amesema upatikanaji wa huduma bora ni muhimu katika kujenga imani ya wananchi kwa mfumo wa afya.

Dkt. Samizi amesisitiza kuwa pamoja na changamoto zilizopo katika mazingira ya kazi za watumishi wa afya, juhudi zinapaswa kuendelea kufanyika katika kuwahamasisha, kuwajengea uwezo na kufuatilia utendaji wao ili kuboresha huduma katika vituo vya afya nchini.