Wizara Ya Afya

TUMEBORESHA HUDUMA ZA AFYA KUELEKEA BIMA YA AFYA KWA WOTE

Posted on: October 22nd, 2026

Na Hassan Kimweri, WAF – Mtwara

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe, amesema Serikali imeendelea kuboresha huduma za afya nchini kwa kuimarisha miundombinu, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kuelekea utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote.

Dkt. Magembe ameyasema hayo leo Oktoba 22, 2026 mkoani Mtwara wakati akitambulisha viongozi walioshiriki katika hafla ya kuanza kwa usajili wa Bima ya Afya kwa Wote Awamu ya Pili ambapo mgeni rasmi ni Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa.

Amesisitiza kuwa uboreshaji wa miundombinu ya kutolea huduma za afya pamoja na upatikanaji wa dawa na vifaa tiba ni sehemu muhimu ya kuhakikisha mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote unakuwa na uwezo wa kuwahudumia wananchi kwa ufanisi.

Aidha, Dkt. Magembe amesema juhudi za Serikali katika kuimarisha sekta ya afya zinalenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa wakati na kwa kuzingatia mahitaji yao, huku mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ukilenga kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma hizo.

Ameeleza kuwa ushiriki wa viongozi na wadau mbalimbali katika hafla hiyo ni muhimu katika kuimarisha uelewa na ushirikiano wa pamoja katika kufanikisha utekelezaji wa mpango huo, ambao unatarajiwa kuongeza fursa kwa wananchi kupata huduma za afya.

Serikali inaendelea kuhamasisha wananchi kushiriki katika usajili wa Bima ya Afya kwa Wote ili waweze kunufaika na huduma za afya kwa mujibu wa utaratibu wa mpango huo bila kuwa na kizwazo cha fedha pindi mtu anapougua.