TMDA YATAJA MAFANIKIO YAKE KATIKA UDHIBITI WA DAWA NA VIFAA TIBA NCHINI
Posted on: October 19th, 2026
Na Happyness Hans, WAF - Dodoma
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Dkt. Adam Fimbo, amesema kuwa Mamlaka hiyo imepata mafanikio mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yake, ikiwemo kuimarisha mifumo ya udhibiti wa dawa na vifaa tiba, kuboresha miundombinu ya maabara na kuongeza mapato, kupitia usimamizi wa Bodi ya Ushauri ya Wizara ya Afya kwa TMDA (MAB).
Akielezea mafanikio hayo leo Oktoba 19, 2026 katika Uzinduzi wa Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa TMDA, Dkt. Fimbo amesema TMDA imefikia daraja la tatu la umahiri duniani katika udhibiti wa Dawa na vifaa tiba huku maabara zake zilizopo Mwanza, Dodoma na Dar es Salaam zikikidhi vigezo vya kimataifa. Aidha, amesema Mamlaka hiyo ina kituo cha umahiri wa ubora wa chanjo barani Afrika, huku ujenzi wa jengo jingine ukiwa katika hatua za mwisho za kukamilika.
Katika kuimarisha miundombinu, Dkt. Fimbo amesema TMDA imejenga tanuru la kuchomea taka katika eneo la Nala jijini Dodoma, Mamlaka hiyo imeendelea kupata hati safi kutoka kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), hali inayoonesha matokeo ya usimamizi wa shughuli zake za kiutendaji na kifedha.
Akizungumzia mafanikio ya kifedha na ukuaji wa sekta ya viwanda, Dkt. Fimbo amesema mapato ya TMDA yameongezeka kutoka shilingi bilioni 40 hadi bilioni 47, huku Mamlaka hiyo ikitoa gawio la shilingi bilioni 21 kwa Serikali. huku idadi ya viwanda imeongezeka kutoka 12 hadi 19, huku TMDA ikiendelea kusimamia na kulinda soko la dawa na vifaa tiba nchini.
Dkt. Fimbo amesema TMDA ilianzishwa mwaka 2003 ikiwa na jina la TFDA kabla ya kubadilishwa na kuwa TMDA. Amesisitiza kuwa lengo kuu la Mamlaka hiyo ni kuhakikisha wananchi wanapata dawa na vifaa tiba vilivyo salama, vyenye ubora na ufanisi, ili kulinda afya za wananchi na kuimarisha ustawi wa jamii.