TANZANIA YASHIRIKI CPHI MILAN 2026 KUVUTIA UWEKEZAJI WA BIDHAA TIBA
Posted on: October 7th, 2026Na WAF–Milan, Italia
Tanzania inashiriki Kongamano na Maonesho ya Kimataifa ya Viwanda vya Dawa, Vifaa Tiba, Chanjo na Vitendanishi (CPHI), linalofanyika Jijini Milan, Italia, kuanzia Oktoba 6–8, 2026.
Chini ya mwavuli wa Kikosi Kazi cha Haraka cha Kuharakisha Uwekezaji katika Sekta ya Dawa na Vifaa Tiba (PIAT), ujumbe wa Tanzania unaongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya anayeshughulikia Dawa na Vifaa Tiba, Bw. Emmanuel Tayari, anayeshiriki katika majadiliano na wadau mbalimbali kuhusu fursa za ubia, uwekezaji na uzalishaji wa bidhaa tiba.
Bw.Emmanuel Tayari amesema kuwa,ushiriki huo umefungua fursa kwa Tanzania kukutana na wawekezaji na wadau mbalimbali wa sekta ya bidhaa tiba duniani, ameeleza lengo ni kuvutia uwekezaji wa ndani na nje na kukuza uzalishaji wa bidhaa tiba nchini.
Aidha,amesisitiza kuwa uwekezaji huo pia unalenga kutangaza fursa zilizopo nchini katika sekta ya bidhaa tiba, ikiwemo uwekezaji katika uzalishaji wa dawa, vifaa tiba, chanjo na vitendanishi, sambamba na kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na wadau wa kimataifa.
Amehitimisha Kwa kueleza kuwa hatua hiyo inaunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya maendeleo ya 2050 kwa kuongeza uzalishaji wa ndani, kupunguza utegemezi wa bidhaa tiba kutoka nje na kuimarisha upatikanaji wa bidhaa tiba bora, salama na zenye ubora kwa ajili ya afya ya jamii.