Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

TANZANIA YARIDHIA MPANGO WA SPPS KUIMARISHA UPATIKANAJI WA BIDHAA ZA AFYA

Posted on: February 21st, 2025

Na WAF - Dar es Salaam

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeridhia Mpango wa Ununuzi wa Pamoja wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Pooled Procurement Services- SPPS) ikiwa ni nyenzo muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya na hivyo kuboresha afya na maisha ya wananchi wote wa nchi wanachama.

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo leo Februari 21, 2025 katika Mkutano wa dharura wa Mawaziri wa Afya na Mawaziri wanaoshughulikia masuala ya VVU na UKIMWI katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), uliofanyika kwa njia ya mtandao akiwa katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya Jijini Dar es Salaam.

“Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaamini kuwa, mpango huu wa pamoja ni nyenzo muhimu ya kutuunganisha katika azma ya jumuiya yetu ya kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya na hivyo kuboresha afya na maisha ya wananchi wetu na umoja wetu ni nguzo muhimu katika kulifikia hilo,” amesema Waziri Mhagama.

Aidha, Waziri Mhagama amesema, katika kuboresha mpango wa biashara uliowasilishwa, Tanzania inapendekeza maboresho madogo ili kuruhusu mifumo mitatu ya ununuzi wa pamoja (hybrid model) kutumika kwa pamoja katika miaka mitano (5) ya kwanza badala ya kuanza na mfumo mmoja tu wa ununuzi wa makundi (group contracting).

“Hatua hii itasaidia kuongeza wigo mpana kwa nchi wanachama kuchagua mfumo itakayoona unafaa kwa mazingira ya nchi yake kwa wakati huo,” amesema Waziri Mhagama.

“Kama tunavyokumbuka, kupitia uamuzi wa mkutano wa Mawaziri wa Novemba 2017, Polokwane, Afrika Kusini, Tanzania iliteuliwa kuwa mwenyeji wa kudumu (host) wa mpango wa ununuzi wa pamoja, hivyo basi, ipo tayari kushirikiana na nchi wanachama pamoja Sekretarieti ya SADC katika utekelezaji wa mpango huo wa ununuzi wa pamoja,” amesisitiza Waziri Mhagama.