Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

TANZANIA YAPIGA HATUA KUPUNGUZA MAGONJWA YANAYOAMBUKIZA

Posted on: June 10th, 2025

Na WAF - Dar es Salaam


Serikali kupitia Wizara ya Afya imepiga hatua ya kupunguza magonjwa ya kuambukiza ikiwemo kiwango cha maambukizi ya VVU kwa watu wenye umri wa miaka 15 na zaidi kutoka asilimia 4.7 mwaka 2016/17 hadi asilimia 4.4 mwaka 2022/23 ikiwa ni mwelekeo sahihi wa kutokomeza maambukizi hayo ifikapo mwaka 2030.


Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo leo Juni 10, 2025 kwenye Mkutano wa tano (5) wa mwaka wa 'Abbott Rapid Diagnostics' unaofanyika jijini Dar es Salaam ambao una lengo la kujadiliana juu ya magonjwa ya kuambukiza uliowashirikisha wajumbe kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki na Kusini. 


Amesema, Tanzania imepiga hatua katika utekelezaji wa malengo ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na UKIMWI (UNAIDS) ya 95-95-95, uwiano wa watu wanaofahamu hali yao ya VVU miongoni mwa wanaokadiriwa kuwa na VVU umeongezeka kutoka asilimia 65 mwaka 2016/17 hadi asilimia 83 mwaka 2022/23. 


"Uwiano wa wanaotumia dawa za kupunguza makali ya VVU umeongezeka kutoka asilimia 94 mwaka 2016/17 hadi asilimia 98 mwaka 2022/23, na waliopata kufubaza virusi (viral suppression) wameongezeka kutoka asilimia 87 hadi asilimia 94 katika kipindi hicho," amesema Waziri Mhagama. 


Aidha, kuhusu homa ya ini, Tanzania imepunguza kiwango cha maambukizi ya Hepatitis B kutoka asilimia 4.3 mwaka 2016/2017 hadi asilimia 3.5 mwaka 2022/2023, na kiwango cha Hepatitis C kimepungua kutoka asilimia 1.1 hadi asilimia 0.2 katika kipindi hicho hicho. 


Kuhusu kutokomeza ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB), Waziri Mhagama amesema idadi ya taarifa za wagonjwa wa TB imeongezeka kutoka elfu 62,180 mwaka 2015 hadi elfu 93,300 mwaka 2023 na kuchangia kupungua kwa asilimia 40 ya ugonjwa huo na asilimia 68 ya vifo katika kipindi hicho. 


"Hii inaonesha kuwa Tanzania iko katika mwelekeo mzuri wa kufikia malengo ya mkakati wa Kimataifa wa kutokomeza ugonjwa wa TB ifikapo mwaka 2030, hii inatokana na kuongeza upatikanaji wa huduma za uchunguzi na kuimarisha mifumo ya afya kwa wananchi," amesema Waziri Mhagama.