Wizara Ya Afya

TANZANIA YAENDELEA KUWA KIVUTIO CHA UWEKEZAJI DUNIANI

Posted on: May 8th, 2026


Kampuni zaidi ya 60 kutoka mataifa mbalimbali Duniani zimeonesha nia ya kuwekeza nchini katika sekta ya dawa, chanjo na vifaa tiba, jambo linaloonesha kuwa Tanzania imeendelea kuaminiwa kama eneo lenye fursa kubwa za uwekezaji na maendeleo ya teknolojia za afya.

Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema hayo leo Mei 08, 2026 wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la uendeshaji wa kongani ya viwanda vya dawa na vifaa tiba katika eneo la Mloganzira Jijini Dar es Salaam akiambatana na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia Mhe. Angela Kairuki.

"Hatua hii kubwa ni ishara kuwa Dunia imeanza kuitazama Tanzania kama kitovu kipya cha uzalishaji wa bidhaa za afya barani Afrika kutokana na mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyojengwa na Serikali, maendeleo endelevu ni kujenga uwezo wa kuzalisha bidhaa kwa ubora na kwa ushindani," amesema Waziri Mchengerwa

Amesema, uwekaji wa jiwe la msingi katika eneo la Mloganzila unaashiria mwanzo wa fikra mpya ya kujenga uchumi wa afya unaotegemea uzalishaji wa ndani wa dawa, chanjo na vifaa tiba badala ya kutegemea bidhaa kutoka nje ya nchi.

"Serikali inalenga kuifanya Tanzania kuwa mshirika wa teknolojia za afya duniani kupitia uwekezaji katika viwanda vya dawa, teknolojia za chanjo pamoja na usindikaji wa kibaiolojia," amesema Waziri Mchengerwa

Aidha, Waziri Mchengerwa amewakaribisha wawekezaji wa ndani na wa Kimataifa kuendelea kuwekeza nchini, akisisitiza kuwa Tanzania ipo tayari kushirikiana nao katika kujenga uchumi wa viwanda na kuongeza uwezo wa uzalishaji wa bidhaa za afya.

Sambamba na hilo, Waziri Mchengerwa amewapongeza wadau wote wa sekta ya viwanda nchini wakiwemo 'Shandong Hongyu Medical Technology Group Co., Ltd' kwa kuwa mwekezaji wa kwanza kuanza ujenzi katika eneo la Mloganzila, akisema hatua hiyo ni ujumbe kuwa utekelezaji wa miradi ya viwanda vya dawa umeanza rasmi.

Mhe. Mchengerwa pia amewapongeza wataalamu wa dawa wa Kitanzania wanaoishi nje ya nchi kwa mchango wao wa kitaalamu katika kuishauri Serikali na kusaidia kuunganisha maarifa, teknolojia na mitandao ya kimataifa kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya