Wizara Ya Afya

TANZANIA YAENDELEA KUIMARISHA HUDUMA ZA LISHE KWA MAMA NA MTOTO

Posted on: June 3rd, 2026

Na Mwandishi wetu Dar es Salaam

Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo "Africa Academy for public health" (AAPH), UNICEF, MUHAS, IHI na TFNC inaendelea kuimarisha juhudi za kuboresha huduma za lishe kwa mama na mtoto kupitia ushirikiano wa kimkakati na wadau mbalimbali wa maendeleo, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha afya bora na ustawi wa wananchi.

Hayo yamebainishwa leo tarehe 03 Juni, 2026 na Mkuu wa Programu ya Uzazi salama, Dkt. Phineas F. Sospeter wakati wa kikao cha kuandaa andiko la mradi wa “Child Nutrition Fund-CNF” lenye lengo la kuimarisha Huduma za Lishe ya Mama na Mtoto hapa nchini.

“Tunafanya kazi kwa karibu na wadau mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha huduma za lishe kwa mama na mtoto zinaendelea kuimarishwa na kuwafikia walengwa kwa ufanisi zaidi,” amesema Dkt. Phineas.

Dkt. Sospeter amesema ushirikiano huo unalenga kuoanisha juhudi za wadau wote wanaofanya kazi katika eneo la lishe ili kuhakikisha afua zinazotekelezwa zinatoa matokeo yanayotarajiwa katika kuboresha afya za mama na watoto.

“Ni muhimu kuwa na mwelekeo mmoja katika utekelezaji wa afua za lishe ili kuhakikisha rasilimali zilizopo zinatumika kwa tija na kuchangia kufikia malengo ya taifa katika kupunguza changamoto za lishe,” amesema Dkt. Sospeter.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za lishe Wizara ya afya, Bi Neema Joshua amesema majadiliano haya yatasaidia kuweka mpango wa pamoja wa utekelezaji na kuongeza fursa za uwekezaji katika afua za lishe kwa mama na mtoto, hatua ambayo itachangia kuboresha afya na ustawi wa jamii kwa ujumla.

Naye Dkt. Rutfild Nnaly kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI amesema kipaumbele kikubwa ni kujenga mifumo endelevu itakayowezesha huduma za lishe kuendelea kutolewa kwa ubora na kwa muda mrefu, huku ikiimarisha upatikanaji wa huduma hizo katika ngazi zote.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Africa Academy for Public Health, Dkt. Mary Mwanyika amesema tunathamini dhamira ya Serikali katika kuweka lishe kuwa miongoni mwa vipaumbele vya afya ya umma.