Wizara Ya Afya

TANZANIA YAANZA SAFARI YA UCHUMI WA AFYA KUPITIA KONGANI YA VIWANDA

Posted on: May 8th, 2026



Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema kuwa Serikali imeanza rasmi safari ya mabadiliko ya kimuundo katika uchumi wa afya nchini kupitia utekelezaji wa mradi wa kongani ya viwanda vya dawa na vifaa tiba katika Hospitali ya Mloganzila, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la maendeleo ya kongani hiyo leo Mei 8, 2026, Mhe. Mchengerwa alisema sekta ya afya haiwezi tena kuonekana kama sekta ya matumizi pekee bali ni sekta muhimu ya uwekezaji, viwanda, teknolojia, ajira, biashara, utafiti na usalama wa Taifa.

“Kupitia mradi huu, Tanzania inaanza safari mpya ya kutoka kwenye utegemezi wa bidhaa za afya kutoka nje kwenda kwenye uzalishaji wa ndani, ubunifu na umiliki wa teknolojia za afya kwa manufaa ya wananchi na uchumi wa Taifa.” amesema Mchengerwa

Mhe.Mchengerwa amesistiza kuwa taifa linalozalisha dawa zake, linalinda maisha ya watu wake,taifa linalotengeneza teknolojia ya afya, linatengeneza mustakabali wake.

“Uzoefu wa janga la UVIKO-19 umeonyesha umuhimu wa nchi kujenga uwezo wa ndani wa kuzalisha dawa, chanjo na bidhaa nyingine za afya ili kukabiliana na changamoto za uhaba, gharama kubwa na kukatika kwa minyororo ya ugavi wakati wa dharura.”amesema Mhe.Mchengerwa

Aidha Mhe.Mchengerwa ameeleza kuwa ajenda ya uwekezaji katika sekta ya afya si ajenda ya Wizara ya Afya pekee, bali ni ajenda ya usalama wa Taifa, uchumi, viwanda, sayansi na diplomasia ya kiuchumi.

“Serikali kupitia PIAT imeamua kutumia mfumo wa “cluster” kwa kuwa sekta ya dawa inahitaji miundombinu maalum, viwango vya juu vya ubora, usalama wa kitaalamu pamoja na mifumo madhubuti ya udhibiti wa uzalishaji.” ameongezea Mhe.Mchengerwa

Mhe.Mchengerwa amesema mfumo huo utawezesha wawekezaji kutumia miundombinu ya pamoja, kupunguza gharama za uwekezaji, kuongeza kasi ya uzalishaji na kuimarisha ushindani wa viwanda vya dawa na vifaa tiba nchini.

“Viwanda havijengi majengo tu; viwanda hujenga uwezo, hujenga nidhamu, hujenga maarifa, na hujenga heshima ya Taifa.” amesistiza Mhe. Mchengerwa.