TANZANIA, WADAU, NCHI JIRANI WAENDELEA KUSHIRIKIANA UBORESHAJI HUDUMA ZA AFYA NCHINI
Posted on: April 29th, 2026Na Hassan Kimweri, WAF - Pwani
Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo pamoja na nchi jirani katika kuimarisha huduma za afya na kudhibiti magonjwa ya mlipuko yanayoweza kuvuka mipaka ya nchi pamoja na utoaji wa chanjo.
Dkt. Magembe amesema hayo leo Aprili 29, 2026 wakati wa maadhimisho ya wiki ya Afya Kitaifa yanayofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani ambapo amesema ushirikiano huo umeendelea kusaidia utekelezaji wa huduma mbalimbali za afya ikiwemo utoaji wa chanjo.
"Maadhimisho ya mwaka huu yamebebwa na kaulimbiu isemayo “Bima ya Afya kwa Wote, Msingi wa Huduma Bora za Afya kwa Kila Mtanzania,” ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya bila vikwazo," amesema Dkt. Magembe
Aidha, Dkt. Magembe amesema Serikali imekabidhi boti saba maalum zitakazotumika kusambaza chanjo na huduma za afya katika maeneo yenye changamoto ya usafiri ambapo boti tano zimepelekwa Tanzania Bara na mbili Zanzibar.
"Katika wiki ya Afya huduma mbalimbali zimetolewa kupitia kliniki tembezi na huduma za mkoba katika zaidi ya vituo 8,600 nchini, huku wananchi wakipatiwa huduma za uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari, shinikizo la damu, saratani pamoja na elimu ya afya," amesema Dkt. Magembe
Pia Dkt. Magembe amesema kuwa Serikali imeendelea kuimarisha usafi wa mazingira kupitia mashindano ya kitaifa ya usafi yaliyohusisha halmashauri, shule, hospitali, vyuo vikuu na taasisi mbalimbali kwa lengo la kuhamasisha jamii kuzingatia kanuni bora za afya na mazingira.
Katika hatua nyingine, Dkt. Magembe amesema Serikali itakabidhi magari maalum yatakayosaidia kusafirisha wagonjwa wanaoshukiwa kuwa na magonjwa ya mlipuko katika maeneo ya mipakani pamoja na vituo vya usafiri wa umma ikiwemo mwendokasi, SGR na vituo vya mabasi.
Mwisho, Dkt. Magembe amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi jirani katika kubadilishana taarifa za afya na kudhibiti magonjwa ya mlipuko kabla hayajasambaa kwa wananchi, huku akiweka wazi kuwa ushirikiano wa kweli unaonekana kupitia huduma zinazowafikia wananchi na jamii zinazolindwa dhidi ya magonjwa.