Wizara Ya Afya

TANZANIA KUPIGA HATUA YA KUJITEGEMEA UZALISHAJI WA DAWA, VIFAA TIBA

Posted on: May 8th, 2026

Tanzania inaendelea kupiga hatua kubwa kuelekea kujitegemea katika uzalishaji wa dawa, chanjo, vifaa tiba na teknolojia za afya, hatua ambayo inalenga kuimarisha uchumi wa ndani na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema hayo leo Mei 08, 2026 wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la uendeshaji wa kongani ya viwanda vya dawa na vifaa tiba katika eneo la Mloganzira Jijini Dar es Salaam akiambatana na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia Mhe. Angela Kairuki.

"Viwanda vya ndani vinapaswa kuandaliwa kufikia viwango vya kimataifa ikiwemo GMP na WHO Pre-qualification ili kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zinakubalika katika masoko ya kikanda na kimataifa," amesema Waziri Mchengerwa

Aidha, Waziri Mchengerwa amesisitiza kuwa uwekezaji katika sekta ya dawa na vifaa tiba si kwa manufaa ya sasa pekee bali ni uwekezaji wa muda mrefu kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.

"Mapinduzi ya teknolojia yanayoendelea duniani kote yanahitaji vijana wa Tanzania na Afrika kuwa sehemu ya suluhisho, si watazamaji, vijana wanapaswa kuwa wabunifu na washiriki wakuu katika maendeleo ya sayansi, teknolojia na uhandisi," amesema Waziri Mchengerwa

Pia, Waziri Mchengerwa amesema Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi, taasisi za elimu na wadau wa maendeleo kuhakikisha uwekezaji katika viwanda vya afya unaendana na utafiti, mafunzo na uendelezaji wa rasilimali watu.

"Tupo tayari kushirikiana na wawekezaji wa ndani na nje katika kujenga uwezo wa uzalishaji wa dawa na vifaa tiba, hatua ambayo inalenga kuifanya nchi kuwa kitovu cha uzalishaji wa bidhaa za afya barani Afrika," amesema Waziri Mchengerwa