Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

TANZANIA, AUDA NEPAD KUSHIRIKIANA MAENEO MATANO SEKTA YA AFYA

Posted on: October 20th, 2024

Na WAF - Dar es Salaam

Serikali kupitia Wizara ya Afya na Wakala wa Maendeleo wa Umoja wa Afrika (AUDA NEPAD) wamesaini makubaliano ya ushirikiano kwenye maeneo matano ya afya ikiwa ni pamoja na kuboresha afya ya uzazi huku Bima ya Afya kwa wote ikiwa ni moja ya mambo yatakayoshugulikiwa.

Makubaliano hayo yamesainiwa leo tarahe 19 Oktoba, 2024 ofisi ndogo za Wizara ya Afya, jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema AUDA NEPAD wako tayari kutoa kiasi cha Dola Milioni Moja (Tsh: bilioni 2.8), zitakazotumika kwenye maeneo ya ushirikiano.

Waziri Mhagama ameeleza kuwa ushirikiano huo pia utawezesha kuwa na wahudumu wa afya ngazi ya jamii wawili kwa kila mitaa, ambao watasaidia kupambana na magonjwa ya milipuko na kupima magonjwa mbalimbali yasiyoambukiza.

Ameongeza kuwa mpaka sasa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imeshapata kiasi cha Dola Laki Tatu kwa ajili ya usimamizi wa kutosha wa usalama wa vifaa vya afya.
"Tunataka kuweka mifumo zaidi ya kusimamia vifaa vya afya na tutahakikisha kwamba malengo yanafikiwa na tukifanya vizuri bidhaa za afya hazitakuwa na maswali," amefafanua Waziri Mhagama.

Waziri Mhagama amesema eneo lingine ni la afya ya uzazi kwa vijana waliopo shule za sekondari ambapo wamepanga kusaidia ili kuepuka mimba zisizotarajiwa kwa vijana hao na kuboresha vituo vya afya ya uzazi, ili kuokoa maisha ya watoto wachanga.

"Vilevile, tumekubaliana kwa pamoja kupambana na unyanyasaji wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto na kutumia akili mnemba katika Sekta ya Afya, hali itakayosaidia wataalamu kushirikiana kwa haraka na minyororo mingi kama dawa, tiba na mengine kufikika kwa urahisi," amesema Waziri Mhagana

Kwa upande wake Afisa Mtendaji MKuu wa AUDA NEPAD Bi. Nardos Bekele amesema, wametenga kiasi cha Dola Milioni 100 kwa ajili ya miradi mbalimbali kwenye nchi za Afrika.