TANGA YAIMARISHA UTAYARI WA JAMII KUKABILIANA NA EL NINO NA UGONJWA WA EBOLA
Posted on: October 8th, 2026Mkoa wa Tanga umeendelea kuimarisha uwezo wa kukabiliana na tishio la ugonjwa wa Ebola na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na El Nino, kupitia Dodoso la maswali lenye tathmini ya mifumo ya mawasiliano ya hatari na ushirikishwaji wa jamii (RCCE) pamoja na (CHMT)katika Wilaya tano za mkoa huo ambazo ni Muheza,Tanga Jiji,Pangani,Korogwe, na Handeni.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo lililofanyika kuanzia Oktoba 5, 2026 hadi Oktoba 7, 2026 Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Bw.Rashid Kassimu Mchatta, amesema Mkoa huo umeendelea kuchukua hatua za tahadhari kwa kuunganisha maandalizi dhidi ya majanga hayo na hatua za kuzuia athari zinazoweza kuchangiwa na mazingira yasiyo salama na alisema miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni kuendesha zoezi la usafi na uzibuaji wa mitaro pamoja na kutoa elimu kwa jamii
“Tunatoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Tanga kuzingatia maelekezo na elimu inayotolewa na wataalamu, kwa sababu ushiriki wa jamii ni sehemu muhimu ya kuzuia na kupunguza athari za majanga,” amesisitiza
Kwa upande wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dkt Japhet Simeo, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa, Dkt Gedion Joshua, amesema maboresho mbalimbali yamefanyika katika sekta ya afya ili kuongeza uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza.
Dkt.Joshua ameeleza kuwa timu za afya zimeandaliwa kutoa huduma na mwitikio pale changamoto zitakapojitokeza, na kusisitiza kuwa tathmini hiyo itasaidia kuangalia maeneo ambayo bado yanahitaji kuimarishwa zaidi katika tahadhari dhidi ya Ebola na athari za El nino.
Aidha, Mratibu wa Elimu ya Afya kwa Umma, Dkt Francis Marwa, amesema jiografia ya Mkoa wa Tanga, ikiwemo uwepo wa mipaka hususani mpaka Mpaka wa Horohoro–Lunga Lunga, unaounganisha Tanzania na Kenya ambao husababisha mwingiliano wa watu,na ni miongoni mwa sababu zinazofanya maandalizi ya mapema kuwa muhimu.
“Tanga ni miongoni mwa mikoa yenye mazingira yanayohitaji tahadhari kutokana na uwepo wa mipaka na mwingiliano wa watu, hivyo uwezo wa kugundua, kutoa taarifa na kuwasiliana na jamii kwa wakati ni muhimu,” amesema Dkt.Marwa