Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

TAASISI LIPENI MADENI YA MSD

Posted on: June 3rd, 2025

Na WAF, DODOMA

Waziri wa Afya Mhe Jenista Mhagama ameziagiza Taasisi zote za Afya zinazodaiwa na Bohari ya Dawa (MSD) kuhakikisha zinalipa madeni kwa haraka ili MSD iweze kujiendesha kwa ufanisi.

Waziri Mhagama ametoa agizo hilo Juni 03, 2025 Bungeni Dodoma wakati akijibu hoja za Wabunge waliotaka kuona MSD inaingia kwenye soko la ushindani kwa kushindana na washitiri wengine.

“Madeni ambayo yapo chini ya fungu 52 (Wizara ya Afya) na mimi mwenyewe ambaye ni Waziri wa fungu 52 tayari tumeshaweka mkataba na Taasisi zote zilipe madeni ya MSD haraka sana,” ameagiza Waziri Mhagama.

Waziri Mhagama amesema kuwa tayari Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) wameshafanya vikao na MSD kwa ajili ya kuweka utaratibu mzuri wa Mamlaka zilizo chini ya OR-TAMISEMI kulipa madeni hayo.

Mapema jana Juni 02, 2025 Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI Mhe. Elibariki Kingu wakati akisoma taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2024/25 alisema kuwa Kamati hiyo imebaini uwepo wa deni la Serikali kwa MSD lenye thamani ya Shilingi Bilioni 434.2.

Mhe. Kingu aliishauri Serikali kuwa ni vyema ikalipa madeni hayo ili kuendelea kuulinda mnyororo wa ugavi na kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kwa wakati na kwa utoshelevu.

Kati ya Shilingi Bilioni 434.2 ambazo MSD inazidai Taasisi za afya, Shilingi Bilioni 46.4 ni kutoka kwenye vituo vya kutolea huduma vilivyopo chini ya Wizara ya afya, Shilingi Bilioni 83.1 kutoka kwenye vituo vya kutolea huduma vilivyopo chini ya OR-TAMISEMI na na Shilingi Bilioni 305 za miradi Misonge.