Wizara Ya Afya

SERIKALI YAWEKEZA BIL. 9.7 KUIMARISHA HUDUMA ZA MOYO JKCI

Posted on: June 12th, 2026

Na Atley Kuni, WAF – Dar es Salaam

Serikali kupitia Wizara ya Afya imezindua rasmi Jengo la Utawala na Vipimo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), hatua inayolenga kuimarisha huduma za kibingwa na kibingwa bobezi nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo Juni 12, 2026, Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema uwekezaji huo unaonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha huduma za afya na kufanikisha malengo ya maendeleo ya taifa kuelekea mwaka 2050.

"Jengo hili limegharimu takribani shilingi bilioni 9.7 na litasaidia kuongeza uwezo wa JKCI kwenye uchunguzi, matibabu na usimamizi wa huduma za moyo, huku akisisitiza kuwa thamani yake halisi ipo katika maisha yatakayookolewa na ubora wa huduma utakaoongezeka", amesema .Mhe. Mchengerwa.

Waziri huyo mwenye dhamani na mambo ya afya amesema, kwa kipindi cha zaidi ya miaka kumi iliyopita, JKCI imekua kutoka kuwa ndoto ya kuwa kituo cha kisasa cha moyo hadi taasisi inayotambulika kimataifa kwa huduma za uchunguzi, upasuaji wa moyo, mafunzo ya wataalamu na tafiti za kisayansi.

Amefafanua kuwa, Sehemu ya uwekezaji huo ni maabara ya kisasa iliyogharimu shilingi bilioni 5.4, yenye uwezo wa kufanya vipimo vya magonjwa ya moyo, damu, figo, homoni na kemia ya mwili kwa viwango vya kimataifa, hivyo kuboresha usahihi wa uchunguzi na matibabu.

Mhe. Mchengerwa amesema maabara hiyo pia imefungwa teknolojia ya Akili Unde (AI) na mifumo ya kisasa ya Automation inayorahisisha uchakataji wa sampuli, kuongeza usahihi wa majibu na kupunguza muda wa kusubiri matokeo ya vipimo.

Aidha, jengo hilo lina huduma za Echocardiographia na X-Ray za kisasa, huku JKCI ikianzisha Health Promotion Studio kwa ajili ya kutoa elimu kwa umma juu ya kinga ya magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo shinikizo la damu, kisukari na magonjwa ya moyo.

Katika hafla hiyo, Waziri Mchengerwa pia amezindua Kijitabu cha Mpango Mkakati wa Safari ya Tanzania kuelekea Huduma za Upandikizaji wa Moyo na kufungua rasmi Bodi ya Wadhamini ya JKCI, hatua zinazolenga kuiwezesha Tanzania kuwa kitovu cha huduma za moyo na tiba utalii katika Afrika Mashariki