Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI YAWEKA MIKAKATI KUDHIBITI KISUKARI

Posted on: October 29th, 2024

Na WAF - Dodoma

Serikali kupitia mkakati wa tano wa Sekta ya Afya (HSSP V) imetangaza mipango na mikakati madhubuti ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza, ikiwemo ugonjwa wa kisukari, kwa kuimarisha elimu kwa umma juu ya njia za kujikinga.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel Oktoba 29, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalum Mhe. Mwantumu Dau Haji, aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto ya ugonjwa sugu wa kisukari nchini.

“Serikali kupitia mkakati wa tano wa Sekta ya Afya imetoa kipaumbele kwa kuweka mikakati madhubuti ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari kwa kuimarisha utoaji wa afua ya elimu kwa umma juu ya kujikinga na ugonjwa huo kama vile kuzingatia ulaji unaofaa, kushughulisha mwili, mazoezi ya viungo pamoja na kuepuka matumizi ya pombe na tumbaku,” amesema Dkt. Mollel.

Aidha, Dkt. Mollel amesema, Sekta ya Afya imetoa kipaumbele kwa kuweka mikakati madhubuti ya kuzuia na kudhibiti magonjwa kwa kuendelea kuimarisha upatikanaji wa dawa, vitendanishi na mashine za kupimia sukari kwa maeneo yote ya kutolea huduma za Afya.

Pia, amesema Serikali inaendelea kutoa mafunzo ya kibingwa kwa wataalamu wa afya juu ya matibabu ya ugonjwa wa kisukari ili kuwawezesha kutoa huduma bora kwa wagonjwa wa kisukari.

Amesema mkakati huo unalenga kukuza ufahamu juu ya ulaji bora, kufanya mazoezi, kuepuka matumizi ya pombe na tumbaku, kuwawezesha watoa huduma kutoa huduma bora kwa wagonjwa wa kisukari na kuboresha mapambano dhidi ya kisukari.