SERIKALI YATOA ONYO: MIWANI NI KIFAA TIBA, SIO BIDHAA YA UREMBO
Posted on: March 27th, 2026Na Mvuda Jaffer, WAF – Dar es Salaam
Serikali kupitia Wizara ya Afya na Baraza la Optometria imewataka wafanyabiashara wa bidhaa za urembo kufuata taratibu na Sheria ya Optometria Sura ya 23, na kuacha kuchanganya bidhaa hizo na vifaa tiba vya macho ili kulinda afya ya watumiaji.
Msajili wa Baraza la Optometria, Bw. Sebastiano Millanzi, ametoa wito huo Machi 27, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya Baraza kufanya usimamizi shirikishi katika vituo vya optometria, zoezi lililofanyika kuanzia Machi 24 hadi 27 katika Manispaa za Temeke, Ubungo na Kigamboni.
Bw. Millanzi amesisitiza kuwa wafanyabiashara hawapaswi kuchanganya bidhaa za urembo kama saa na bidhaa nyingine na vifaa tiba vya optometria kama miwani tiba, fremu za miwani na miwani ya kuzuia mwanga, kwani hali hiyo inaweza kusababisha mkanganyiko kwa watumiaji.
Ameeleza kuwa wafanyabiashara wote wanaouza bidhaa za optometria wanapaswa kuwa na cheti halali cha usajili kutoka Wizara ya Afya kupitia Baraza la Optometria.
Aidha, Bw. Millanzi amesema Baraza linaendelea kushirikiana na mamlaka nyingine ili kuhakikisha watoa huduma wanazingatia sheria na miongozo ya utoaji wa huduma za macho kwa lengo la kulinda afya ya mwananchi.
Katika ziara hiyo, Baraza lilibaini changamoto kadha katika utoaji wa huduma za macho kwenye kliniki za optometria na vituo vingine vya afya, ikiwepo pamoja na baadhi ya wafanyabiashara kuuza miwani tiba, fremu na miwani ya kuzuia mwanga kinyume na Sheria ya Optometria Sura ya 23, jambo linaloweza kuhatarisha afya ya jamii.
Bw. Millanzi ameongeza kuwa baadhi ya wafanyabiashara wanaendesha biashara kwa leseni zisizokidhi vigezo, huku wengine wakitoa dawa kinyume na masharti ya usajili. Pia, baadhi ya vituo vimeanza kutoa huduma kabla ya kukamilisha usajili, na baadhi ya wataalamu wamekiuka wigo wa kazi zao.
Ameiasa jamii kuepuka kununua miwani kiholela na badala yake kufuata huduma hizo katika vituo vinavyotambulika na kusajiliwa na Wizara ya Afya.
Kwa mujibu wa Bw. Millanzi, Baraza lilitembelea jumla ya vituo 47, ambapo kliniki za optometria zilikuwa 14 na vituo vya kusambaza vifaa tiba vya optometria vilikuwa 33.